Tracy Wanjiku: Mwanadada wa miaka 23 anayetazamia kumbwaga chini Ruto katika uteuzi wa UDA

Muhtasari

•Tracy Wanjiku Kingoli  ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT) ameashiria azma yake ya kukabiliana na Ruto na Orina katika kinyang'anyiro cha tiketi ya UDA.

•Kwa kuwa Wanjiru ana ulemavu wa miguu hatahitajika kutoa shilingi milioni moja ambazo kila mgombea urais kwa tikiti ya UDA anahitajika kutoa.

Image: FACEBOOK// UNITED DEMOCRATIC ALLIANCE

Asubuhi ya Jumamosi chama cha United Democratic Alliance (UDA) kiliandaa kikao cha mahojiano na uhakiki wa wagombea urais ambao wanawania tikiti ya chama.

UDA ambacho kitakuwa chama kipya katika uchaguzi wa mwezi Agosti kiliwapokea wagombea urais watatu ambao wanamezea tikiti hiyo.

Kando na naibu rais William Ruto, Bw Orina Jephanai na  mwanadada mwenye umri wa miaka 23 pia walialikwa kwenye mahojiano hayo.

Tracy Wanjiku Kingoli  ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT) ameashiria azma yake ya kukabiliana na Ruto na Orina katika kinyang'anyiro cha tiketi ya UDA.

Siku ya Alhamisi , chama hicho kiliwaandikia watatu hao barua kikiwaalika kwa mahojiano na uhakiki katika makao yake makuu ya Hustler Plaza. 

"Wagombea urais wa UDA; Naibu Rais William Samoei Ruto, Bi Tracy Wanjiru na Bw Orina Jephanei wamealikwa kwa mahojiano ya uteuzi katika Hustler Plaza Jumamosi," Taarifa ya chama hicho ilisoma.

Watatu hao walihitajika kufika mbele ya kamati ya uteuzi Jumamosi wakiwa wamebeba vitambulisho, pasipoti, thibitisho ya malipo ya uteuzi, hati za masomo na wasifu wao.

Kwa kuwa Wanjiru ana ulemavu wa miguu hatahitajika kutoa shilingi milioni moja ambazo kila mgombea urais kwa tikiti ya UDA anahitajika kutoa.

Chama cha UDA kinapanga kutangaza mpeperusha bendera wake kwenye uchaguzi wa urais katika Kongamano la Wajumbe wa Kitaifa litakalofanyika Machi 15.