"Baba aliponiona alisema kwao hakuzaliwi watoto kama mimi," Isaac Mwaura afunguka kuhusu utoto wake mgumu

Muhtasari

•Mwaura alisema alilelewa na mamake pekee baada ya babake kumkana hata kabla ya kupata fursa ya kujuana.

•Kutokana na hali yake ya uzeruzeru alipelekwa katika shule maalum ya watoto wenye matatizo ya kuona akiwa na umri mdogo wa miaka minne.

• Alifichua kuwa watu walimkejeli sana kutokana na maumbile yake na wengine hata kuwa na hamu ya kumguza kwa udadisi tu.

Image: FACEBOOK// ISAAC MWAURA

Seneta mteule Isaac Mwaura amefichua muwa babake alijitenga naye punde baada yake kuzaliwa takriban miongo minne iliyopita.

Akiwa kwenye mahojiano na Ala C katika kipindi cha Reke Ciume na Ene, Mwaura alisema alilelewa na mamake pekee baada ya babake kumkana hata kabla ya kupata fursa ya kujuana.

Alisema babake hakuridhishwa na maumbile yake akaibua madai kuwa hakuna uwezekano wa mtoto kama yeye kutoka kwa familia yao.

"Nyumbani kwetu asili  ni Githunguri. Hata hivyo nimelelewa Githurai. Mama alikuwa anafanya kazi ya kuunda chaki kwa kampuni iliyokuwa Ruiru. Baba aliponiona alisema kwao hakuzaliwi watoto wanaofanana na Mwaura. Mimi ni mtoto wa mama single ," Mwaura alisimulia.

Mgombeaji huyo wa ubunge wa Ruiru katika uchaguzi wa Agosti alieleza kuwa mamake alichukua majukumu yote ya malezi baada ya babake kuwatoroka.

Kutokana na hali yake ya uzeruzeru alipelekwa katika shule maalum ya watoto wenye matatizo ya kuona akiwa na umri mdogo wa miaka minne.

"Nilipelekwa katika shule ya bweni nikiwa na miaka minne unusu. Nilipelekwa Shule ya Vipofu ya Thika kwa kuwa nilizaliwa nikiwa tofauti. Tukiangalia sasa haikuwa na haja. Ni vizuri lakini kwa kuwa labda ningechokozwa sana na watoto wengine katika shule za kawaida," Alisema.

Mwanasiasa huyo alisema alikumbana na changamoto nyingi alipokuwa akikua. Alifichua kuwa watu walimkejeli sana kutokana na maumbile yake na wengine hata kuwa na hamu ya kumguza kwa udadisi tu.

"Watu walikuwa wananiambia ningepelekwa hospitali mapema nibadilishwe damu ili niwe weusi. Watu walikuwa wanakuja kwetu kunitazama wakishangaa mimi ni mtoto wa aina gani. Walikuwa wanaongea Kikuyu wakidhani siwasikii. Wengine hata walikuwa wanataka kunigusa ngozi. Hali ilikuwa ngumu," Mwaura alisema.

Alisema hali ya kuwa mtoto asiyefahamu mengi kuhusu yaliyokuwa yanaendelea ilimsaidia kustahimili kejeli  za watu.

Mwaura pia alifichua kuwa mamake hakupendelea kuzungumzia suala la mzazi mwenzake ambaye aliwakimbia punde alipozaliwa. 

Licha ya changamoto zilizomkabili utotoni, Mwaura aliweka wazi kuwa alilelewa katika mazingira ya upendo nyumbani kwao.