•Hakimu wa mahakama ya Milimani Martha Nanzushi aliwaachilia 16 hao Jumatatu baada ya DPP kusema hawakupata ushahidi wa kutosha kuwahusisha na kosa hilo.
•Mshukiwa mkuu wa tukio hilo Zachariah Nyaore Obadiah, hata hivyo atashtakiwa leo.
Image: DOUGLAS OKIDY
Mahakama imewaachilia washukiwa 16 waliokuwa wamezuiliwa kutokana na video inayosambaa ya dereva wa kike akinyanyaswa katika Barabara ya Wangari Maathai.
Hakimu wa mahakama ya Milimani Martha Nanzushi aliwaachilia 16 hao Jumatatu baada ya DPP kusema hawakupata ushahidi wa kutosha kuwahusisha na kosa hilo.
Upande wa mashtaka ulisema afisa wa upelelezi hakupata ushahidi unaowahusisha washukiwa hao na kesi ya unyanyasaji wa kijinsia mnamo Machi 4.
“Kutokana na afisa mpelelezi kukosa ushahidi wa kuwafungulia mashtaka watuhumiwa, ninawaachilia chini ya kifungu cha 87 (a) cha Kanuni ya Adhabu”, Hakimu aliamuru.
Aliagiza washukiwa warudishwe katika kituo cha polisi cha Gigiri ili kuchukua simu zao na mali zao nyingine.
Mshukiwa mkuu wa tukio hilo Zachariah Nyaore Obadiah, hata hivyo atashtakiwa leo.
Upande wa mashtaka ulisema wana ushahidi wa kutosha wa kumshtaki na Zachariah katika kesi ya shambulio hilo.
Washukiwa hao walikuwa wamekaa rumande kwa zaidi ya siku 15 wakisubiri uchunguzi.