Hatujaficha pesa zozote, wandani wa Ruto wasema

D8D4RU_X4AAhEO.jfif
D8D4RU_X4AAhEO.jfif
Wanasiasa wanaomuunga mkono Naibu Rais William Ruto wamesema hawana hofu na hatua ya serikali kutangaza kusitisha matumizi ya noti za sasa za shilingi elfu moja ifikiapo Oktoba tarehe moja. Walisema hatua hiyo itaondoa madai kuwa wameficha mamilioni ya pesa za ufisadi katika nyumba zao na ambazo wamekuwa wakitoa makanisani kwa harambee kile wikendi.

Wanasiasa hao akiwemo Gavana wa Kiambu Ferdinad Waititu ambaye amehojiwa na Tume ya kupambana na ufisadi EACC walikuwa wakizungumza kataika kanisa eneo la Kahawa Wendani, Kaunti ya Kiambu.

Wanasiasa hao waliokuwa wameandamana na Naibu Rais William Ruto waliitaka Serikali kupunguza muda wa kuondolewa kwa noti ambazo zimekuwepo za elfu moja kutoka tarehe iliyowekwa ya Oktoba mosi.

“Hatua hii ingechukuliwa kitambo sana ili kukabili ulaghai wa kifedha nchini,” Mbunge wa South Mugirango Sylvanus Osoro alisema.

Wanasiasa hao vile vile waliunga mkono agizo la rais Uhuru Kenyatta kutaka serikali kulipa madeni ya watu na makampuni yaliotoa huduma kwa serikali kabla ya mwisho wa kipindi hiki cha kifedha mwezi Juni.

Pia walisema kwamba kutolipwa kwa wafanyibishaa na serikali kumeathiri sana ukuaji wa biashara nchini, hususan biashara ndogo na za kadri.

Walizungumza siku ya Jumapili katika kanisa la Kahawa eneo Bunge la Ruiru walipotaka serikali kutilia maanani maslahi ya wafanyibiashara wadogo.