Kenya yafikisha watu 582 walioambukizwa virusi vya Corona-Mutahi

EXVfIylVAAAklZ3
EXVfIylVAAAklZ3
NA NICKSON TOSI

Kenya imesajili maambukizi mapya 47 ya virusi vya corona na kufikisha jumla ya watu 582 waliothibitishwa kuambukizwa maradhi haya.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe amesema kuwa serikali pia imewaruhusu watu wengine 8 kurudi nyumbani baada ya kupona virusi vya corona kufikisha watu waliopona nchini kuwa 192. Aidha Kagwe amesema watu wawili wameaga dunia na kufikisha watu 26 walioaga dunia.

Wakati huo huo Kagwe amesema serikali imepiga marufuku ya kuingia na kutoka mitaa ya Eastleigh hapa Nairobi na Old Town Mombasa kwa siku 15 kuanzia leo ( Jumatano) jioni saa moja ili kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo.

Shughuli za kibiashara na zinginenezo katika maeneo hayo zitafungwa kuanzia hii leo.

Visa hivyo vipya 47 vimetokea maeneo yafuatayo;  32 - Mombasa, 11 - Nairobi, 2 - Busia, 1 - Kiambu 1 - Kwale.

Mutahi pia amesema usafiri wa magari ya umma katiki maeneo ya Eastleigh na Old Town umepigwa marufuku.

Waziri pia amewaonya watu wanaouza vifaa maalum vya kujikinga ambavyo vinastahili kutumiwa na wahudumu wa afya (PPE) wakati wanaposhughulikia wagonjwa wa virusi vya corona.

Serikali pia imetangaza kwamba madereva wa masafa marefu watafanyiwa vipimo saa 48 kabla ya kuingia nchini na kuwasilisha stakabadhi za kuonyesha upimaji huo.

Vile vile madereva hao watakuwa wanafanyiwa vipimo kila baada ya siku 14.

Serikali pia imewapunguza wafanyakazi wa bandari nchini ili kuzuia maambukizi miongoni mwa watu.