Kila kitu unachohitaji kujua kuhusu mechi ya Kenya dhidi ya Uganda

Tikiti za mechi ya kirafiki kati ya Harambee Stars na Uganda zitaanza kuuzwa jumapili asubuhi.

Tikiti hizo zitauzwa shilingi 200 na zitapatikana katika maeneo haya; mkabala na hoteli ya Safari Park, kituo cha polisi cha Ngomongo na nje ya Gate 12 ya uwanja wa Kasarani.

Mechi hii itaanza saa kumi kamili. Stars wanajitayarisha kwa michuano ya kufuzu kwa kombe la dunia la CAF itakayoanza mwezi Novemba. Hii itakua mechi ya kwanza ya kocha mpya Francis Kimanzi.

Hata hivyo, Kimanzi amesema mechi ya kirafiki dhidi ya Uganda ni fursa nzuri ya kuwajaribu wachezaji wapya katika timu ya kitaifa. Kimanzi aliyepewa cheo hicho baada ya Sebastien migne kufutwa kazi anasema ana hamu ya kuwaona wachezaji wa humu nchini wakipambana na Uganda.

Timu hiyo itakuwa bila wachezaji Victor Wanyama, Johanna Omolo, Joseph Okumu, Abud Omar na Ismael Gonzalez.

Hayo yakijiri, FKF imethibitisha kua Harambee Stars itachuana na Msumbiji kabla ya kuanza kampeni yao ya kufuzu kwa Afcon mwaka 2021.

Mwenyekiti wa FKF Nick Mwendwa amefichua kua mechi hii imepangiwa kuchezwa baada ya timu hio kupambana na Libya katika mechi nyingine itakayochezwa Morocco Oktoba tarehe 11.

Kenya, ambao wako katika kundi G, wataanza kampeni hio kwa kuchuana na Misri Novemba tarehe 1 jijini Cairo. Togo na visiwa vya Comoro ziko kwenye kundi moja na Kenya.