Maambukizi ya ukimwi yaongezeka kaunti ya Busia

Viwango vya maambukizi ya maradhi ya ukimwi vimeongezeka katika kaunti ya Busia kwa muda wa miaka michache iliopita.

Haya yamefichuliwa na mshirikishi wa baraza la kupambana na ukimwi NACC kanda ya magharibi Steve Kathaka na mkurugenzi wa matibabu kaunti ya Busia dakt. Melisa Lutomia wakati wa hafla ya kuwahamasisha viongozi wa wahudumu wa bodaboda 60 kuhusu maradhi ya ukimwi.

Wawili hao wametaja kaunti ya Busia kuwa kwenye mpaka wa Kenya na Uganda kama moja wapo ya sababu kuu ambazo zinachangia ongezeko hilo huku wakielezea mikakati ambayo wameweka kukabiliana na maambukizi hayo.

Aidha wameungana na viongozi wa wahudumu wa bodaboda kuwarai wanabodaboda kujitokeza na kujua hali yao ya afya mbali na kujiepusha na mienendo inayoweza pelekea wao kuambukizwa maradhi hayo.

Hayo yakijiri, viongozi wa kidini kaunti ya Taita Taveta hii leo wameandaa kikao na gavana wa kaunti hiyo Granton Samboja ili kushinikiza maridhiano Kati yake na wawakilishi wadi.

Wakiongozwa na askofu wa kianglikana Liverson Ng’onda, wamemrai Samboja kushirikiana na viongozi wengine ili kufanikisha maendeleo katika kaunti hiyo.