Mamia ya wafanyikazi wa vyuo vikuu kupoteza kazi

magoha
magoha
Mamia ya wafanyikazi watapoteza kazi wakati serikali itaanza kutekeleza pendekezo la waziri wa Elimu George Magoha kuvifunga baadhi ya vyuo vikuu nchini. Serikali hata hivyo imesema zoezi hilo litatekelezwa kwa njia ya utu.

Hatua ya kufunga baadhi ya vyuo vikuu vya umma na kuunganisha baadhi yavyo inalenga kuimarisha viwango vya elimu nchini.

“Taasisi zitakazosalia zitakuwa zinazalisha watahiniwa wenye ujuzi unaohitajika katika soko la kazi,” waziri wa elimu George Magoha alisema.

Magoha alisema serikali inataka taasisi za elimu ya juu nchini kuheshimiwa kote ulimwenguni. Hili linaweza tu kuafikiwa kwa kutathmini shughuli za vyuo vikuu nchini, kozi zinazo tolewa na kama zina manufaa.

“Tunataka kuhakikisha kwamba katika kipindi cha kati ya miaka 10 – 20 tutakuwa na vyuo vikuu ambavyo vitazalisha wanafunzi wanaohitajika katika dunia yenye teknojia ya kisasa” alisema siku ya Jumanne mjini Naivasha alipofungua kongamano kuhusu ugaidi katika vyuo vikuu iliyoandaliwa na kituo cha kitaifa cha kukabiliana na ugaidi.

Waziri alihusisha changamoto zinazotokana na ugaidi kwa ufisadi na mipaka ya Kenya inayovuja na kuruhusu magaidi huingia nchini kupitia njia za mkato, kutekeleza uhalifu na kuua wananchi wasiokuwa na hatia.