Hongera! Mwanariadha Ferdinand Omanyala aivunja tena rekodi ya Kenya katika mbio za mita 100

Omanyala amekuwa Mkenya wa kwanza kumaliza mbio hizo chini ya sekunde 10 baada ya kukimbia kwa sekunde 9.86 akiwa nchini Austria siku ya Jumamosi.

Muhtasari

•Dakika chache kabla ya kuandikisha rekodi hiyo Omanyala tayari alikuwa ameivunja rekodi mpya aliyoandikisha Tokyo kwa kumaliza na sekunde 9.96.

•Rekodi ya dunia katika mbio hizo kwa sasa inashikiliwa na Usian Bolt wa Jamaica ambaye aliwahi kukimbia kwa sekunde 9.58, nukta sekunde 28 tu chini ya rekodi ya Omanyala.

Ferdinand Omanyala aonyesha rekodi yake mpya
Ferdinand Omanyala aonyesha rekodi yake mpya
Image: TWITTER

Mwanariadha Ferdinand Omurwa Omanyala ameivunja tena rekodi ya Kenya katika mbio za mita 100 takriban wiki mbili baada ya kuweka rekodi mpya ya sekunde 10 katika michuano ya Olimpiki iliyofanyika jijini Tokyo, Japan.

Omanyala amekuwa Mkenya wa kwanza kumaliza mbio hizo chini ya sekunde 10 baada ya kukimbia kwa sekunde 9.86  akiwa nchini Austria siku ya Jumamosi.

Dakika chache kabla ya kuandikisha rekodi hiyo Omanyala tayari alikuwa ameivunja rekodi mpya aliyoandikisha Tokyo kwa kumaliza na sekunde 9.96.

Rekodi ya dunia katika mbio hizo kwa sasa inashikiliwa na Usian Bolt wa Jamaica ambaye aliwahi kukimbia kwa sekunde 9.58, nukta sekunde 28 tu chini ya rekodi ya Omanyala.

Akisherehekea fanikio hilo kwenye ukurasa wake wa Twitter, Omanyala ambaye alionekana kajawa na bashasha alidai kuwa matokeo hayo yalikuwa ya kushangaza kwake  pia na kusema kwamba anatazamia kufanya zaidi atakapokuwa Helsinki, Finland.

"Ati nini!!! mtu aniambie eti sio ndoto. Hii itafahamika miaka mingi baadae. Shukran @fitnessfromafrica, @Odibetskenya, @usnkenya na Andorf Austria. Kwenye hatua nyingine. Tuonane hivi karibuni Helsinki, Finland.  Maisha marefu kwa nafasi za pili" Omanyala alisema.

Wakenya wengi wameendelea kumbubujikia Omanyala sifa na pongezi anapojivunia matokeo hayo ya kuridhisha.