Mike Tyson: Naona mwisho wa maisha yangu duniani hivi karibuni

Bondia Tyson alifana sana katika mashindano mwishoni mwa miaka ya tisini na mwanzo wa miaka ya 2000.

Muhtasari

• Tyson alisema umaarufu na utajiri ndio ulifanya yeye kuharibu maisha yake na kusema sasa hana haja na mali ya duniani kama pesa na vitu vingine.

• Alisema kila mara anapojitazama kwenye kioo huona madoa na kujisemea kwamba mwisho wake umekaribia.

Bondia wa zamani wa Marekani Mike Tyson
Bondia wa zamani wa Marekani Mike Tyson
Image: screenshot//YouTube

Mwanamsaumbwi mkongwe kutoka Marekani Mike Tyson ameushangaza ulimwengu baada ya kudai kwamba kila mara anapotafakari kuhusu maisha yake siku hizi, anaona ni kama mwisho wake kuwa duniani unakaribia na unakuja kwa kasi mno.

Katika moja ya podcast zake za ‘Hotboxin’ With Mike Tyson’ aliyoipakia kwenye ukurasa wake wa YouTube wiki moja iliyopita, Tyson akizungumza na daktari wake mtaalamu wa afya pamoja na mwanaume mwingine, alisema kwamba huwa anajiangalia kwenye kioo na kuoa makunyanzi, mapeto na madoadoa ya majeraha usoni mwake na kujisemea kimoyomoyo kwamba siku zake duniani zinakaribia kikomo.

Tyson mwenye umri wa miaka 56 anasema kwamba pindi anapojitazama kweney kioo anaona kwamba baadhi ya viungo vyake vya mwili na haswa usoni vinazidi kudorora, jambo lilaloashiria kwamab huenda akaondoka kwenye uso wa dunia hivi karibuni zaidi.

“Sisi sote tutakufa siku moja bila shaka. Ninapojitazama kwenye kioo, naona madoa hayo madogo usoni mwangu, nasema, wow! Hiyo inamaanisha kuwa tarehe yangu ya kumalizika kwa muda wangu duniani inakaribia, hivi karibuni,” Tyson alisema kwa ujasiri na ukakamavu usoni mwake.

Katika maongezi hayo ya kipekee yenye uhuru wa kuzungumza wa aina yake, Tyson pia alizungumzia maisha yake kwa undani na kugusia kiasi jinsi anavyoyaona maisha haswa kuelekea ‘mwisho wake duniani’ ambapo alisema kwamba hata amefikia kiwango ambapo hana haja tena na mali ya duniani kama pesa, majumba makubwa na hata magari.

“Pesa haimaanishi kitu kwangu. Mimi huwaambia watu kila wakati, wanafikiri pesa itawafurahisha, hawajawahi kuwa na pesa hapo awali - unapokuwa na pesa nyingi, huwezi kutarajia mtu yeyote kukupenda. Nitakirije mapenzi yangu kwako wakati una $500 bilioni? Unaamini hakuna kinachoweza kutokea. Huamini kwamba benki zinaweza kuanguka. Unaamini kwamba huwezi kushindwa wakati una pesa nyingi, ambayo si kweli. Ndio maana huwa nasema pesa ni hisia potofu za usalama,” Tyson alizungumza kwa ukakasi mwingi.

Mike Tyson alikwa bondia miaka ya tisini na kuelekea miaka ya awali ya 2000 ambapo mapambano yake mengi aliyashinda kwa mkumbo wa kwanza na hivyo kujijengea heshima ya kudumu haswa kutoka kwa Wamarekani.