Tottenham yamteua aliyekuwa kocha wa Wolves, Nuno Santo kama kocha mkuu

Tottenham imempatia Mreno huyo mkataba wa miaka miwili hadi mwaka wa 2023.

Muhtasari

•Nuno atakuwa anajaza pengo ambalo liliachwa baada ya klabu hiyo ya jiji la London kupiga kalamu aliyekuwa kocha wake,  Jose Mourinho mwezi wa Aprili. 

•Kocha huyo alisaidia Wolves kurejea kwenye ligi kuu ya Uingereza(EPL) mwaka wa 2018 baada ya kushinda taji la Championship katika msimu wa 2017/18. Aliipia klabu hiyo uongozi bora huku wakimaliza katika nafasi ya saba katika misimu ya kwanza miwili baada ya kurejea EPL.

Nuno Espirito Santo baada ya kuteuliwa Tottenham
Nuno Espirito Santo baada ya kuteuliwa Tottenham
Image: Twitter//Tottenham

Klabu ya Tottenham imemteua aliyekuwa kocha wa Wolverhampton Wandererers (Wolves) Nuno Espirito Santo kama kocha  mkuu .

Tottenham imempatia Mreno huyo mkataba wa miaka miwili hadi mwaka wa 2023.

Nuno atakuwa anajaza pengo ambalo liliachwa baada ya klabu hiyo ya jiji la London kupiga kalamu aliyekuwa kocha wake,  Jose Mourinho mwezi wa Aprili. Wadhifa huo umekuwa ukishikiliwa na Ryan Glen Mason.

Nuno ambaye katika miaka yake ya ujana alicheza kama mlinda lango alimaliza mkataba wake na klabu ya Wolves mwisho wa msimu wa 2020/21. Alikuwa mkufunzi katika timu ya Wolves kwa kipindi cha miaka minne.

Kocha huyo alisaidia Wolves kurejea kwenye ligi kuu ya Uingereza(EPL) mwaka wa 2018 baada ya kushinda taji la Championship katika msimu wa 2017/18. Aliipia klabu hiyo uongozi bora huku wakimaliza katika nafasi ya saba katika misimu ya kwanza miwili baada ya kurejea EPL.

Kando na Wolves, Nuno aliwahi kuwa mkufunzi katika klabu ya Rio Ave ya Ureno, Valencia ya Uhispania na Porto ya Ureno.

Mmilikaji wa Tottenham, Daniel Levy alimsifia kocha huyo na kueleza imani yake kuwa ataweza kuletea timu hiyo matokeo bora

"Unahitaji tu kuangalia kipindi Nuno alichokuwa pale Wolves uone uwezo wake kuchukua kikosi cha wachezaji na kutekeleza mtindo wa kucheza ambao unaleta matokeo bora na unawezesha wachezaji kustawi" Levy alisema.

Nuno kwa upande wake alieleza furaha yake kwa uteuzi huo na kuahidi kuwa atatekeleza kazi yake vilivyo.

"Ni raha kubwa kuwa hapa na natazamia sana kuanza. Hatuna siku za kupoteza na sharti tuanze kufanya kazi mara moja kwani mechi za  matayarisho ya msimu ujao zinatarajiwa kuanza hivi karibuni" Nuno alisema.

Msimu uliopita, klabu ya Tottenham ilimaliza katika nafasi ya saba na pointi 62.