EURO 2020

Rashford aomba msamaha kwa kukosa penati, agoma kuomba msamaha kwa rangi yake

Marcus Rashford ni mmoja wa wachezaji watatu wa England waliopoteza penati

Muhtasari

•Rashford anasema hayo kufuatia kusakamwa na kubaguliwa kwa misingi ya rangi baada ya yeye na wenzake Bukayo Saka na Jadon Sancho kukosa penati katika mchezo wa fainali ya Euro 2020 dhidi ya Italia, uliomalizika kwa England kuchapwa kwa mikwaju ya penati 3-2 baada ya mchezo kumalizika kwa sare ya 1-1

•Nahodha wa England Harry Kane amewaambiA wote walio nyuma ya udhalilishaji wa kibaguzi dhidi ya Rashford, Sancho ana Saka: " Wewe sio mshabiki wa England na hatukuhitaji'

Mchoro wa picha ya Marcus Rashford ukiwa na ujumbe wa kuunga mkono juhudi zake liliharibiwa lakini imeregeshwa Jumatano
Mchoro wa picha ya Marcus Rashford ukiwa na ujumbe wa kuunga mkono juhudi zake liliharibiwa lakini imeregeshwa Jumatano
Image: REUTERS

Mshambuliaji wa England Marcus Rashford ameomba msamaha kwa kukosa penati lakini anasema 'sitaomba msamaha kwa jinsi nilivyo'.

Rashford anasema hayo kufuatia kusakamwa na kubaguliwa kwa misingi ya rangi baada ya yeye na wenzake Bukayo Saka na Jadon Sancho kukosa penati katika mchezo wa fainali ya Euro 2020 dhidi ya Italia, uliomalizika kwa England kuchapwa kwa mikwaju ya penati 3-2 baada ya mchezo kumalizika kwa sare ya 1-1

Wachezaji wote hao watatu wamekuwa wakisakamwa kupitia mitandao ya kijamii tangu kumalizika kwa fainali hizo.

"Namna nlivyojisikia ni kama nimemuangusha kila mtu," Rashford aliandika kwenye taarifa yake hiyo.

Nyota huyo wa Manchester United mwenye umri wa miaka 23 aliongeza: "naweza kukubali kukosolewa kwa kiwango changu, penati yangu haikuwa nzuri, ingeweza kujaa wavuni, lakini kamwe siwezi kuomba msahama kwa namna nilivyo na kwa asili yangu'

Marcus Rashford ni mmoja wa wachezaji watatu wa England waliopoteza penati.

Jumatatu hii kocha wa England Gareth Southgate alisema ubaguzi wa rangi ni jambo lisilosamehewa huku waziri mkuu wa nchi hiyo, Boris Johnson na chama cha soka cha England wakikemea vitendo hivyo.

Polisi wameanza kufanya uchunguzi na kusisitiza jambo hilo haliwezi kuvumiliwa.

"Hata sijui wapi pa kuanzia na sijui nielezeje kwa namna navyojisikia wakati huu. Nimekuwa na msimu mgumu, nafikiri hilo liko wazi kwa kila mtu na pengine nmeenda kwenye fainali nikiwa sijiamini sana. Mara zote nimekuwa najiamini kwenye penati, lakini mambo hayakwenda sawa.

Mambo mengi yalikuwa yanazunguka kichwani kwangu, na pengine hakuna neno lolote linaloweza kuelezea hali inavyokuwa. Fainali. Miaka 55. Penati 1. Historia. Nachoweza kusema tu ni samahani. Natamani mambo yangekuwa tofauti.

Mimi ni Marcus Rashford, mtu mweusi mwenye miaka 23 kutoka Withington & Wythenshawe, Kusini mwa Manchester. Kama sina kitu kingine basi najivunia hicho. Kwa meseji njema zote nazotumiwa, naweza kusema nashukuru. Nitarejea nikiwa na nguvu zaidi. Tutarejea tukiwa na nguvu zaidi."

Bukayo Saka ni miongoni mwa wachezaji walioshambuliwa kwa misingi ya ubaguzi wa rangi mitandaoni
Bukayo Saka ni miongoni mwa wachezaji walioshambuliwa kwa misingi ya ubaguzi wa rangi mitandaoni
Image: reuters

Ukubwa wa tatizo la ubaguzi wa rangi

Chama cha wachezaji wa kulipwa nchini England (PFA) kinasema takwimu zilizotolewa kupitia Channel 4 news baada ya kumalizika kwa mashindano ya Euro 2020 kunaonyesha kwamba kuna zaidi ya tweets 850,000 tweets zilizohusu mashindano hayo zilichambuliwa na kuonyesha yafuatayo:

  • 1,913 zilikuwa za kudhalilisha, zikiwalenga Sancho, Saka, Rashford na Raheem Sterling.
  • Machapisho 167 kwenye mtandao wa twitter zilikuwa na maneno makali zaidi ya kudhalilisha.

PFA ilisema, wakati baadhi ya tweets hizi zikifutwa, akaunti bado hazijaondolewa kabisa na Twitter.

"Uchambuzi wetu wa awali unaonyesha kwamba udhalilishaji mwingi uliofanyika kwenye fainali za Euro 2020, ukiwalenga Jadon Sancho, Bukayo Saka, Marcus Rashford na Raheem Sterling, ulikuwa mkubwa zaidi ukilinganisha na udhalilishaji wa matukiomengine yote ukiyajumlisha.

Mtandao wa Twitter ulisema umefuta machapisho zaidi ya 1,000 katika kipindi cha saa 24 na kuzifungia akaunti kadhaa zilizokiuka sheria na kanuni za mtandao huo.

Wachezaji wa Italia na England wakipiga goti katika fainali ya Euro 2020
Wachezaji wa Italia na England wakipiga goti katika fainali ya Euro 2020
Image: HISANI

'Nyie sio mashabiki wa England na hatuwahitaji'

Nahodha wa England Harry Kane amewaambiA wote walio nyuma ya udhalilishaji wa kibaguzi dhidi ya Rashford, Sancho ana Saka: " Wewe sio mshabiki wa England na hatukuhitaji'

Mshambuliaji huyo wa Tottenham ameongeza kwenye mtandao wa Twitter: "Wanastahili kuungwa mkono, sio kufanyiwa vitendo vya kibaguzi vilivyoanza tangu usiku. Kama unamtukana na kumbagua mtu kwneye mitandao ya kijamii, wewe sio shabiki wa England na soka."

Mchezaji wa England Tyrone Mings akiwa mazoezini
Mchezaji wa England Tyrone Mings akiwa mazoezini
Image: HISANI

Kiungo wa England Kalvin Phillips alisema alichukizwa na vitendo hivyo vya kibaguzi vilivyoelekezwa kwa wachezaji hao wenzake. "Hakuna kitu kingine isipokuwa upendo na heshima kwa ndugu zangu kwa ujasiri wao," aliandika.

Historia ya ubaguzi

Ubaguzi katika soka sio jambo geni.

Winga wa zamani wa John Barnes aliwahi kueleza alivyopitia ubaguzi hasa wa rangi katika maisha yake ya soka.

"Kumbukumbu ya jambo hili ipo kwa muda mrefu," Barnes aliiambia BBC mwaka 2018, kufuatia tukio linguine la ubaguzi wa rangi dhidi ya Raheem Sterling.

"Kwa mchezaji mweusi katika miaka ya 1980 mambo yalikuwa yale yale ya nyimbo za kibaguzi, kurushiwa ndizi uwanjani, kili kilichoonekana kuwa sehemu ya jamii na soka."

Jadon Sancho pia ameshambuliwa kupitia mitandao ya kijamii baada ya kukosa penati Jumapili
Jadon Sancho pia ameshambuliwa kupitia mitandao ya kijamii baada ya kukosa penati Jumapili
Image: REUTERS

Jadon Sancho pia ameshambuliwa kupitia mitandao ya kijamii baada ya kukosa penati Jumapili.

Kwa Barnes, ubaguzi katika michezo ni sehemu tu ya tatizo. Ambalo ni kubwa.

"Sahau kuhusu soka, tunapaswa kuacha kulitenga hili, na kufikiri kwamba ni tatizo katika mpira wa miguu na kwingine ni hakuna tatizo," alisema.

"Tunapaswa kulitazama hili kwa ukubwa wake, na tupambane kwa ujumla dhidi ya ubaguzi wa rangi katika maisha. Ukifanya hivyo utaondoa tatizo hilo kwenye soka."

Wakati tatizo la ubaguzi wa rangi likiendelea katika mpira wa miguu, lakini vitendo vya kibaguzi vilishuka katika miaka ya 1980s - kwa mujibu wa Prof Ellis Cashmore, mwanasosholojia na mtaalam wa ubaguzi katika soka, kutoka chuo kikuu cha Aston, Uingereza.

"Leo ubaguzi hauwezi kukaribia kiwancho kilichokuwepo katika miaka ya 1980s cha kushangaza bado vinaendelea kuwepo katika mchezo huu'.

"Lakini katika soka, inaonekana kuna utamaduni uliweka mizizi wa ubaguzi," alisema.