Christiano Ronaldo, Mikel Arteta wapokea tuzo za mchezaji na meneja bora mwezi Septemba

Muhtasari

•Raia huyo wa Ureno ameweza kuonyesha umahiri wake kwenye ulingo wa kandanda kwa kushinda tuzo la mchezaji bora katika mwezi wake wa pili tu baada ya kurejea EPL.

•Licha ya kuwa na mwanzo mbaya wa msimu wa EPL 2021/22, meneja wa Arsenal Mikel Arteta aliweza kushinda tuzo la meneja bora wa mwezi wa Septemba.

INSTAGRAM

Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) imetangaza matokeo ya meneja bora, mchezaji bora na bao bora la mwezi Septemba.

Mshambulizi matata wa Manchester United Christiano Ronaldo ametangazwa kama mchezaji bora wa mwezi Septemba baada ya kufunga mabao matatu katika mechi tatu za EPL ambazo alishiriki.

Raia huyo wa Ureno ameweza kuonyesha umahiri wake kwenye ulingo wa kandanda kwa kushinda tuzo la mchezaji bora katika mwezi wake wa pili tu baada ya kurejea EPL.

Ronaldo alifunga mabao mawili katika mechi dhidi ya Newcastle United mnamo Septemba 11 huku bao la tatu akifunga kwenye mechi dhidi ya WestHam mnamo Septemba 19.

Wachezaji wengine ambao walikuwa wameteuliwa kushinda tuzo hilo ni pamoja na beki wa Manchester City Joao Cancelo, beki wa Chelsea Antonio Rudiger, mshambulizi wa Newcastle  Allan Saint-Maximin, Ismaila Sarr  wa Watford na and mshambulizi  Mohamed Salah wa Liverpool.

Ronaldo alishinda tuzo la mchezaji bora wa EPL mara ya mwisho mwezi Machi mwaka wa 2008 kabla ya kuondoka United kuelekea Real Madrid.

Licha ya kuwa na mwanzo mbaya wa msimu wa EPL 2021/22, meneja wa Arsenal Mikel Arteta aliweza kushinda tuzo la meneja bora wa mwezi wa Septemba.

Arteta aliweza kunyakua taji hilo baada ya timu yake kushinda mechi zote tatu za  EPL, kufunga mabao matano na kutofungwa kwenye mechi mbili.

Raia huyo wa Uhispania aliweza kutoa timu klabu yake kutoka nafasi ya mwisho hadi nafasi ya 11 ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.

Mameneja wengine ambao walikuwa wameteuliwa kuwania tuzo hilo ni pamoja na Pep Guardiola wa Manchester City, Jurgen Klopp wa Liverpool, Graham Potter wa Brighton na Dean Smith wa Aston Villa.

Winga wa Everton Andros Townsend alishinda tuzo la bao la mwezi kufuatia bao murua ambalo alifunga kwenye mechi dhidi ya Burnley mnamo Septemba 13.