EPL 2021/22: Matokeo ya raundi ya 9, Hali ilivyo kwenye jedwali

Muhtasari

•Vijana wa Ole Gunnar Solskjær walionyeshwa kivumbi nyumbani kwao huku wakishambuliwa kwa mabao manne katika kipindi cha kwanza na kuongezwa la tano bila jawabu  katika kipindi cha pili. 

•Kwa sasa The Blues wanaongoza jedwali na pointi 22 huku wakifutwa na Liverpool, Mancity na West Ham ambao wameandikisha pointi 21, 20 na 17 mtawalia kufikia sasa.

Image: TWITTER/ LIVERPOOL

Raundi ya tisa ya michuano  ya EPL iling'oa nanga usiku wa Ijumaa huku jumla ya mechi kumi zikichezwa katika nyanja mbalimbali nchini Uingereza kwa kipindi cha siku tatu 

Mechi ya ufunguzi kati ya Arsenal na Aston Villa ilichezwa mida ya saa nne unusu usiku wa Ijumaa ugani Emirates..

Wanabunduki waliweza kuonyesha makali yao kwa kuwapiga vijana wa Dean Smith 3-1 nyumbani licha ya kuandikisha matokeo hafifu  dhidi  yao msimu uliopita. Mabao ya Thomas Partey, Pierre-Emerick Aubameyang na Emile Smith Rowe yalipatia klabu hiyo ya London ushindi huku Jacob Ramsey akifungia Villa bao la kufutia machozi.

Michuano ya raundi ya tisa iliendelea siku ya Jumamosi huku mechi sita za kusisimua zikichezwa.

Mechi ya kusisimua zaidi na ambayo ilishuhudia mabao mengi kati ya Chelsea na Norwich ugani Stamford Bridge ilifungua ratiba ya Jumamosi.

Miamba hao wa soka kutoka London walipata ushindi mkubwa zaidi kuwahi shuhudiwa msimu huu baada ya kuwalaza Norwich mabao 7 bila jawabu. Hat-trick ya Mason Mount, bao la kujifunga la Max Aarons na mabao ya Calum Hudson-Odio, Recce James, Ben Chilwell yalipatia mabingwa hao wa Champions League ushindi.

Mechi nne zaidi zilichezwa mwendo wa saa kumi na moja jioni ambapo ushindi mmoja na sare tatu zilishuhudiwa.

Mechi kati ya Leeds na Wolves na ile ya Crystal Palce dhidi ya Newcastle ziliishia sare ya 1-1 huku mechi kati ya Southampton na Burnley ikiandikisha sare ya 2-2.

Mchuano kati ya Everton na Watford ulishuhudia mabao saba huku tano yakiwa ya wageni Watford huku wenyeji wakiweza kufunga mawili tu. Licha ya vijana wa Rafa Benitez kutangulia kufunga katika dakika ya tatu, Watford waliweza kuamka na kutia wavuni mabao matano ikiwemo hat-trick ya mshambulizi Joshua King.

Mechi ya mwisho siku ya Jumamosi ilikuwa kati ya Brighton na washindi wa EPL msimu uliopita Manchester City.

Vijana wa Guardiola waliweza kuwika ugenini  1-4 kupitia mabao ya Ikay Gundogan, Phil Foden (2) na Riyad Mahrez. Bao la pekee la Brighton lilifungwa na Mac Alister kupitia mkwaju wa penalti.

Mechi tatu zaidi  zilichezwa siku ya Jumapili huku mechi kati ya Manchester United na Liverpool iliyokuwa imesubiriwa kwa hamu na ghamu ikichezwa mwendo wa saa kumi na mbili unusu ugani Old Trafford

Vijana wa Ole Gunnar Solskjær walionyeshwa kivumbi nyumbani kwao huku wakishambuliwa kwa mabao manne katika kipindi cha kwanza na kuongezwa la tano bila jawabu  katika kipindi cha pili. Mshambuliza nyota wa Liverpool Mohammed Salah alifunga hatrick huku  Diogo Jota na Naby Keita wakiongeza chumvi kwenye kidonda cha United.

Hapo awali Leicester walishinda 2-1 ugenini dhidi ya Brentford huku Westham wakipata ushindi wa 1-0 nyumbani dhidi ya Tottenham

Kwa sasa The Blues wanaongoza jedwali na pointi 22 huku wakifutwa na Liverpool, Mancity na West Ham ambao wameandikisha pointi 21, 20 na 17 mtawalia kufikia sasa.

Nafasi tatu za mwisho zinashikiliwa na Burnley, Newcastle na Norwich ambao wako na pointi 4, 4 na 2 mtawalia.