Shabiki sugu wa Simba ajitoa uhai siku ya mechi, aacha ujumbe azikwe na jezi ya klabu hiyo

Muhtasari

•Marehemu aliacha kama ameandika ujumbe kwa karatasi akiomba kuzikwa kama mwili wake umevalishwa jezi ya Simba  kutokana na upendo mkubwa aliokuwa nao kwa klabu hiyo.

•Mnamo siku Khalfan alijitia kitanzi Simba ilipoteza 0-1 dhidi ya Mbeya City na wengi waliamini kwamba marehemu aliamua kujitoa uhai kutokana na mafadhaiko 

Image: SIMBA FC TANZANIA

Klabu ya soka ya Tanzania, Simba imeomboleza mmoja wa mashabiki wake sugu ambaye anaripotiwa kujitoa uhai mnamo Januari 17.

Khalfan Mwambena 17, ambaye alikuwa mkazi wa jiji la Mbeya alijitia kitanzi siku ya mechi kati ya Simba na Mbeya City FC.

Polisi jijini Mbeya wamethibitisha kwamba Mwambena alijitoa uhai kabla ya mechi hiyo wala si baada ya mechi hiyo kama ripoti za hapo awali zilivyokuwa zinadai.

Marehemu aliacha kama ameandika ujumbe kwa karatasi akiomba kuzikwa kama mwili wake umevalishwa jezi ya Simba  kutokana na upendo mkubwa aliokuwa nao kwa klabu hiyo.

"Naipenda sana Simba, I love you Simba na nikifa nizikwe na jezi ya Simba" Ujumbe ulioachwa na marehemu ulisoma.

Klabu ya Simba pamoja na mashabiki wamemuomboleza marehemu na kuitakia roho yake ilazwe mahali pema peponi.

"Khalfan ameonyesha mapenzi makubwa kwa Simba, Tunamuomba Mungu ailaze roho yake mahala pema peponi" Taarifa ya Simba inasoma.

Mnamo siku Khalfan alijitia kitanzi Simba ilipoteza 0-1 dhidi ya Mbeya City na wengi waliamini kwamba marehemu aliamua kujitoa uhai kutokana na mafadhaiko yaliyomkumba baada ya klabu aliyoipenda sana kupokea kichapo.

Hata hivyo Simba imepuuzilia mbali ripoti hizo.