AFCON: Mbwembwe za Gideon na Kalonzo zafurahisha mitandaoni

Muhtasari

• Vinara wa muungano wa OKA, Gideon Moi na Kalonzo Musyoka walichachisha mitandaoni Usiku wa Februari 6, wakati wa mechi ya fainali ya ubingwa wa Afrika, AFCON baina ya Senegal na Misri.

• Gideon Moi alikuwa akiwapigia upato Misri kuibuka mabingwa na kuinyuka Senegal huku kwa upande wa pili Musyoka akiwa nyuma ya Senegal

Gideon Moi na Kalonzo Musyoka
Image: Facebook

Vinara wa muungano wa OKA, Gideon Moi na Kalonzo Musyoka walichachisha mitandaoni Usiku wa Februari 6, wakati wa mechi ya fainali ya ubingwa wa Afrika, AFCON baina ya Senegal na Misri.

Viongozi hao waliwapakulia wakenya furaha isiyo na kifani pale walipoanzisha mbwembwe za kuchekesha, kila mmoja akivutia upande wa timu aliyokuwa akiipigia upato kuibuka bingwa katika kipute hicho kilichowakutanisha washambuliaji wa timu ya Liverpool, Sadio Mane na Mohammed Salah.

Gideon Moi alikuwa akiwapigia upato Misri kuibuka mabingwa na kuinyuka Senegal huku kwa upande wa pili Musyoka alikuwa nyuma ya Senegal ambao wamefika katika fainali za dimba hilo kwa mara ya pili mtawalia.

Katika mbwembwe zake, Moi aliandika kwenye mtandao wa Facebook kuwa liwe liwalo Mo Salah na timu yake ya Misri lazima wangeshinda na kumtaka Musyoka kukubali matokeo mapema.

“Hadi mchezo huu utakapokamilika, Mo Salah na timu yake watakuwa wanatembea kwenye bahari ya Shamu, na hata Mane hatoweza kumsimamisha,” Moi alipandisha mbwembwe.

Kwa upande wake, Musyoka alimtania Moi kwamba Mane na timu ya Senegal watatawanyisha maji ya bahari ya Shamu na kuiacha Misri nyuma.

Mechi hiyo ilikamilika baada ya matuta ya penati ambapo Senegal waliibuka mabingwa na ikabidi Moi kuwa mnyenyekevu huku Musyoka akibaki na sauti ya kumtaka Moi ampe jogoo.

"Hili ni hakikisho la kitakachotokea Agosti 9. Maji ya bahari ya Shamu yameshatawanyishwa na tunavuka ng'ambo ya pili. Leta kuku wangu Gideo Moi," aliandika Musyoka.

Wengi wa mashabiki wa vinara hao wamefurahishwa na utani waoo huku wengine wakiwataka kuleta mihemko kama hiyo katika soka la Kenya.