Mashetani Wekundu wapewa mkono wa kwaheri Champions League

Muhtasari

•Nafasi ya vijana hao wa Ragnick kutwaa kombe la kwanza ndani ya kipindi cha miaka 5 ilififia baada ya kupokea kichapo cha 0-1 nyumbani.

•Atletico inajumuika na Bayern Munich, Manchester City, Benfica,Liverpool na Real Madrid ambao tayari wamehitimu kuingia robo fainali ya Champions League

Manchester United imebanduliwa kutoka Champions League
Manchester United imebanduliwa kutoka Champions League
Image: GETTY IMAGES

Usiku wa Jumanne Klabu ya Manchester United ilioneshwa mlango wa kutokea Ligi ya Mabingwa ( UEFA Champions League)  na mabingwa wa Uhispania msimu uliopita Atletico Madrid.

Mashetani wekundu walikuwa na nafasi finyu ya kupenya kuingia robo fainali ya kombe hilo baada ya kutoka sare ya 1-1 katika raundi ya kwanza iliyochezwa mwezi jana.

Nafasi ya vijana hao wa Ragnick kutwaa kombe la kwanza ndani ya kipindi cha miaka mitano hata hivyo ilififia baada ya kupokea kichapo cha 0-1 nyumbani.

Beki Renan Lodi alifungia Atletico bao la pekee katika dakika ya 41.

Kuondoka kwa United kutoka Champions League kunamaanisha kuwa sasa watang'ang'ania tu kuboresha nafasi yao kwenye EPL katika juhudi za kufuzu kwa kombe lolote la Ulaya msimu ujao.

Atletico inajumuika na Bayern Munich, Manchester City, Benfica,Liverpool na Real Madrid ambao tayari wamehitimu kuingia robo fainali ya Champions League.