Orodha ya mataifa yatakayowakilisha Afrika katika Kombe la Dunia

Muhtasari

•Mechi tano za fainali ya kufuzu kwa kombe la kimataifa zilichezwa usiku wa Jumanne ambapo orodha rasmi ya mataifa yatakayoshiriki ilitolewa.

•Ni rasmi kwamba Senegal, Ghana, Cameroon, Morocco na Tunisia zitapeperusha bendera ya Afrika katika mashindano hayo.

Image: TWITTER// FOOTBALL SENEGAL

Hatimaye mataifa matano ambayo yatawakilisha Bara Afrika katikaKombe la Dunia la mwaka huu nchini Qatar yamethibitishwa.

Mechi tano za fainali ya kufuzu kwa kombe la kimataifa zilichezwa usiku wa Jumanne ambapo orodha rasmi ya mataifa yatakayoshiriki ilitolewa.

Senegal ilifuzu baada ya kutimua Misri kupitia matuta ya penalti. Sadio Mane alifungia taifa lake penalti ya ushindi baada ya Misri kushindwa kufunga penalti tatu kati ya nne za kwanza. 

Ghana ilifuzu baada ya kutoka sare ya 1-1 na Nigeria ugenini. Mechi ya mkondo wa kwanza kati ya mataifa hayo mawili iliishia sare tasa.

Cameroon ilipata ushindi wa 2-1 ugenini dhidi ya Algeria na kujipatia nafasi katika Kombe la Dunia litakalochezwa mwezi Novemba.

Morocco ilifuzu baada ya kucharaza Congo DRC kwa mabao 4-1. Mechi ya mkondo wa kwanza ilikuwa imeishia sare ya 1-1.

Tunisia pia iliweza kujinyakulia nafasi katika kombe hilo baada ya kuandikisha sare ya 0-0 na Mali. Katika mechi ya mkondo wa kwanza Tunisia iliweza kuchapa Mali 1-0.

Ni rasmi kwamba Senegal, Ghana, Cameroon, Morocco na Tunisia zitapeperusha bendera ya Afrika katika mashindano hayo.