"Kurudisha mkono wa shukrani" Dennis Oliech aanzisha wakfu wa kukuza vipaji vya vijana wasiojiweza nchini

Muhtasari

• Dennis Oliech - "Wakfu wa Dennis Oliech utakuza vipaji vya vijana kutoka kwa wasiojiweza katika jamii, na kuunda mwamko wa kijamii na kiuchumi katika jamii pamoja,”

Mshambuliaji wa Harambee Stars, Dennis Oliech
Mshambuliaji wa Harambee Stars, Dennis Oliech
Image: Facebook

Mchezaji wa zamani wa soka Dennis Oliech ametangaza kuzindua wakfu wa kusaidia watu wasiojiweza na pia kukuza talanta ya michezo humu nchini.

Akiweka tangazo hilo wazi kupitia ukurasa wake wa Facebook Jumatatu, staa huyo matata aliyewarambisha garasa mabeki enzi zake uwanjani alisema kwamba wakfu wake kwa jina Dennis Oliech Foundation utazingatia kuinua vipaji haswa vya soka nchini kama njia moja ya kudumisha mchezo wa kandanda nchini Kenya.

“Kutokea katika hali duni na upendo kwa jamii yangu na Kenya kwa ujumla siku zote umekuwa mkubwa na sasa ni wakati wangu wa kurudisha mkono wa shukrani kwa jamii, wakati wangu wa kufanya zaidi na kugusa maisha ya vijana wengi wa Kenya ambao wangependa kuwa kama mimi na hata kufikia zaidi ya nilivyofanya katika shughuli zote za michezo. Wakfu wa Dennis Oliech utakuza vipaji vya vijana kutoka kwa wasiojiweza katika jamii, na kuunda mwamko wa kijamii na kiuchumi katika jamii pamoja,” alitangaza mshambuliaji huyo matata.

Oliech alianza taaluma yake ya soka katika klabu ya Dagoretti Santos jijini Nairobi kabla ya kujiunga na timu ya Mathare United na baadaye kutanua mbawa zake kimataifa ambapo alitua katika ligi ya Qatar, baadae Ufaransa na kisha kumalizia Dubai alikokipiga na vilabu vingi tu vya mchezo wa kandanda.

Mchexaji huyo alikuwa nahodha wa timu ya taifa ya Harambee Stars kwa michezo 76 ambapo alikuwa mfungaji bora wa muda wote.