Tajiri Namba Moja Duniani Elon Musk Adokeza Kununua Manchester United

Tajiri huyo miezi kadhaa nyuma pia alidokeza nia yake ya kuununua mtandao wa Twitter.

Muhtasari

• Musk, Mkurugenzi Mtendaji wa magari ya umeme ya Tesla, alitoa tangazo la ujasiri kwa wafuasi wake milioni 103 kutangaza nia yake ya kuinunua Manchester United Jumatano alfajiri.

Tajiri namba moja duniani Elon Musk adokeza kununua Man United
Tajiri namba moja duniani Elon Musk adokeza kununua Man United
Image: Facebook//Fabrizio Romano

Mwanaume namba moja kwa utajiri kote duniani mzaliwa wa Afrika Kusini, Elon Musk amejulikana kuchochea mambo kwenye mtandao wa Twitter mara kwa mara, na alijitosa katika ulimwengu wa michezo katika suala hilo Jumanne usiku.

Musk, Mkurugenzi Mtendaji wa magari ya umeme ya Tesla, alitoa tangazo la ujasiri kwa wafuasi wake milioni 103 kutangaza nia yake ya kuinunua Manchester United Jumatano alfajiri.

“Ili kuwa wazi, ninaunga mkono nusu ya kushoto ya Chama cha Republican na nusu ya kulia ya Chama cha Kidemokrasia! Pia, ninainunua Manchester United, karibu!” Musk aliandika kwenye Twitter yake.

Tagazo hili lisilojulikana kama ni la ukweli ama ni utani wake wa kila muda lilipokelewa kwa maoni mseto huku wengi wa waliouona wakisema Tajiri huyo anafanya mzaha na wataamini tu ile siku atawasilisha dau mezani.

Musk alitoa matamshi haya yake baada ya klabu hiyo ya Uingereza kuwa na mwanzo mbaya katika kampeni za msimu huu kusaka ubingwa wa EPL baada ya kukaa kweney kijibaridi kwa zaidi ya miaka 10 sasa.

United walianza kwa kupigwa mara mbili mfululilo na timu zinazokisiwa kuwa na ubora wa nusu jedwali na mpaka sasa timu hiyo ni miongoni mwa zile zinazoburura mkia bila pointi wala bao hata moja licha ya kuwa timu iliyokuwa inaogopewa miaka michache iliyopita.

Familia ya Glazer, ambayo pia inamiliki Buccaneers ya NFL, ndiyo wanahisa wanaodhibiti sasa wa Manchester United, na mashabiki wengi wameandamana katika miaka ya hivi karibuni kujaribu kuwashinikiza waiuze timu hiyo huku ikiendelea kuyumba katika kutokuwa na umuhimu.