Saudi Arabia yatangaza sikukuu ya likizo baada ya kuishinda Argentina kombe la dunia

Saudi Arabia iliishinda Argentina 2-1 katika mechi ya kufungua kampeni zao kutafuta ubingwa wa kombe la dunia.

Muhtasari

• Ushindi wa ajabu wa timu ya taifa ya kandanda ulionekana kama ushindi uwanjani na wakati mkubwa kwenye jukwaa la michezo la kimataifa.

Wachezaji wa Saudi Arabia wakisujudu baada ya kipenga cha mwisho. Walishinda Argentina 2-1
Wachezaji wa Saudi Arabia wakisujudu baada ya kipenga cha mwisho. Walishinda Argentina 2-1
Image: Hisani

Mfalme wa nchi ya Saudi Arabia, Salman ametangaza Jumatano Novemba 23 kuwa sikukuu ya likizo kufuatia timu ya taifa hilo kuichachafya Argentina katika mechi ya kombe la duni inayoendelea nchini Qatar.

Katika taarifa iliyopeperushwa na vyombo vya habari vya kimataifa, mfalme Salman alisema kuwa ushindi huo ni mkubwa sana kwa taifa lake na hivyo hakuna shughuli rasmi itakayofanyika Jumatano, shule zote na taasisi zote za kiserikali zitasalia kufungwa huku taifa hilo likisherehekea kuibwaga Argentina iliyokuwa inajivunia mchezaji bora duniani, Lionel Messi.

Saudi Arabia ilirejea baada ya kufungwa penalti ya mapema ya Lionel Messi na kusababisha mshtuko mkubwa kabisa wa Kombe la Dunia kutokana na bao la kusawazisha la Saleh Al-Shehri na bao la ushindi la Salem Al-Dawsari kwenye Uwanja wa Lusail mjini Doha.

“Sherehe zilizuka kote katika mji mkuu wa Riyadh baada ya filimbi ya mwisho kupulizwa, huku mashabiki wakiunda duru za dansi zisizotarajiwa na kupeperusha bendera ya taifa yenye upanga kutoka kwenye madirisha ya magari yaendayo kasi,” moja ya jarida la India liliripoti.

Ushindi wa ajabu wa timu ya taifa ya kandanda ulionekana kama ushindi uwanjani na wakati mkubwa kwenye jukwaa la michezo la kimataifa, ambapo mamlaka hiyo ya kikanda kwa muda mrefu imekuwa ikitafuta nafasi ya kuangaziwa.

Likizo hiyo itakuwa ya wafanyikazi wote wa serikali "na sekta ya kibinafsi, na wanafunzi wa kiume na wa kike katika hatua zote za elimu", serikali ilitangaza Jumanne jioni.