Beki wa Arsenal, Ben White aondoka Qatar kwa sababu za kibinafsi

Wakati huo huo, Uingereza imeratibiwa kumenyana na Senegal katika raundi ya mtoano.

Muhtasari

• Nyota huyo wa zamani wa Brighton alitajwa kama mchezaji wa akiba katika mechi mbili za ufunguzi.

Ben White, beki wa Uingereza na Arsenal
Ben White, beki wa Uingereza na Arsenal
Image: FA//Twitter

Beki wa Arsenal, Ben White ameripotiwa kuondoka katika kambi ya timu ya taifa ya Uingereza nchini Qatar huku mashindano ya kombe la dunia yakiwa yanaendelea.

Kulingana na jarida la The Sun, White aliondoka kambini na kurejea zake nyumbani Uingereza katika ile alikitaja kuwa sababu za kibinafsi na hawezi kurudi tena Qatar.

Beki huyo wa kati ya Arsenal alijumuishwa katika kikosi cha wachezaji 26 waliotajwa na kocha Gareth Southgate lakini tangu mashindano ya kombe la dunia yang’oe namga wiki mbili zilizopita, White hajapata kucheza hata sekunde moja.

Sports Brief Kenya walieleza kuwa Nyota huyo wa zamani wa Brighton alitajwa kama mchezaji wa akiba katika mechi mbili za ufunguzi za England dhidi ya Iran na Marekani lakini alishindwa kuingia kwenye kikosi katika mechi ya mwisho ya Kundi B dhidi ya Wales.

Kuondoka kwake kunatajwa kuwa huenda ni kughadhabishwa na pia kutamaushwa baada ya kukosa nafasi ya kuwakilisha Uingereza uwanjani hata sekunde moja katika mashindano hayo makubwa zaidi ulimwenguni.

Maendeleo hayo yalithibitishwa na FA, ambao walifichua kwamba mchezaji huyo aliondoka kwa sababu za kibinafsi na hakuna uwezekano wa kurejea.

Wakati huo huo, Uingereza imeratibiwa kumenyana na Senegal katika raundi ya mtoano, huku Gareth Southgate akitarajiwa kushirikiana na Harry Maguire na John Stones katika kiini cha safu yake ya ulinzi.