Mbappe aandikisha rekodi mpya Kombe la dunia, awapiku Zidane, Henry, Platini

Alifunga mabao mawili na kuisaidia Ufaransa kuwa timu ya kwanza kutimba kwenye hatua ya 16 bora.

Muhtasari

• Hii ni mara yake ya pili kushiriki katika michuano ya kombe la dunia na tayari amefunga mabao 7, mawili zaidi kumliko Thierry Henry aliyeshiriki mashindano ya kombe la dunia mara 4.

Kiungo mshambuliaji wa Ufaransa, Kylian Mbappe.
Kiungo mshambuliaji wa Ufaransa, Kylian Mbappe.
Image: Getty Images

Timu ya taifa ya Ufaransa kwa mara nyingine tena iliandikisha rekodi baada ya kuwa mabingwa watetezi wa kombe la dunia wa kwanza tangu Brazil mwaka 2006 kufuzu kwenye hatua ya 16 bora katika mashindano hayo yanayoendelea nchini Qatar.

Ufaransa ilikuwa timu ya kwanza kabisa kutimba kwenye hatua ya 16 bora ya mashindano hayo yanayoendelea katika taifa hilo la Mashariki ya kati.

Ufaransa walijihakikishia nafasi hiyo baada ya kuinyuka Denmark mabao mawili kwa moja, mabao yote ya Ufaransa yalitiwa wavuni na kinda wa PSG, Kylian Mbappe.

Baada ya Mbappe kufunga mabao hayo mawili na kuiwezesha Ufaransa kuingia hatua ya 16 bora, mabao hayo yalimaanisha kitu kikubwa sana kwa kinda huyo mwenye umri wa miaka 26 tu.

Mwanzo, Mbappe ambaye ni mara yake ya pili kushiriki mashindano yenye haiba ya juu kama hayo sasa amefikisha mabao 7 jumla na hivyo kuvunja rekodi za baadhi ya wababe wa michezo waliowahi kushiriki mashindano hayo mbele yake.

Mbappe sasa ana upungufu wa bao moja tu nyuma ya wachezaji mastaa Lionel Messi na Christiano Ronaldo ambao wameshiriki mashindano hayo kwa mara kadhaa na wote wana mabao 8 kila mmoja. Ikumbukwe wawili hao wana miaka zaidi ya 30 kwenda juu ilhali Mbappe ni kinda tu wa miaka 23!

Rekodi nyingine kubwa kabisa ambayo mchezaji huyo aliandikisha ni kuwa baada ya kufunga mabao mawili, sasa ana mabao mengi zaidi kumliko aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa Ufaransa na Barcelona, Thiery Henry ambaye alishiriki katika mashindano ya kombe la dunia mara nne.

Henry ana mabao 6 baada ya mashindano ya kombe la dunia mara nne huku Mbappe akiwa na mabao 7 katika mashindano ya kombe la duni mara 2.

Kando na Henry, Mbape pia amewapita miamba wa Ufaransa, Zidane, Platini ambao wana mabao 5 kila mmoja.