"Yaliyopita si ndwele, hatumfukirii hata kidogo!" - Ten Hag ajibu kuhusu Ronaldo

Ronaldo walitofautiana vikali na Ten Hag kupelekea kuondoka kwake Old Trafford kwa njia ya kishari mno.

Muhtasari

• Tangu kuondoka kwake Old Trafford, Ronaldo alikuwa mchezaji huru mpaka aliposaini na Al Nassr.

Ten Hag akinong'onezana na Ronaldo
Ten Hag akinong'onezana na Ronaldo
Image: The Guardinan

Meneja wa timu ya Manchester United, Eric Ten Hag ameendeleza mashambulizi yake dhidi ya aliyekuwa mchezaji wa timu hiyo, Christiano Ronaldo baada ya kutofautiana vikali mwezi Novemba kupelekea mkataba wa Mreno huyo kukatishwa na United.

Ronaldo katika mahojiano yaliyozungumziwa mno Novemba mwaka jana, aliwatuhumu watu wengii katika timu ya United huku akidhihirisha wazi kuwa katu hawezi kuwa na heshima kwa kocha Ten Hag katika kile alisema kuwa Mholanzi huyo hakuwa anamuonesha heshima na kwa hivyo naye akaamua kulipa kwa kutomheshimu.

Tangu hapo, Ten Hag amekuwa akikwepa suala la kuzungumzia Ronaldo katika kile kinaonekana kuwa suala lolote kuhusu Mreno huyo linamchefua pakubwa.

Mwishoni mwa mwaka jana, Ronaldo alijipatia mkataba mnono na timu ya Al Nassr inasyoshiriki ligi kuu ya Saudi Arabia, jambo ambalo limemfanya kuzungumziwa pakubwa kwenye mitandao ya kijamii.

Baada ya kumalizika kwa mechi ya United dhidi ya Wolves ambayo ndio ilikuwa ya kufunga mwaka, United waliibuka washindi kwa bao moja komboa ufe na meneja Ten Hag alipoulizwa mwishoni mwa mechi hiyo hisia zake kuhusu hatua ya Ronaldo kuelekea Saudia, alijibu kwa jeuri na kejeli akisema kuwa katu hawezi kuzungumzia mambo ambayo yamepitwa na wakati na badala yake kumtaka mwanahabari kuuuliza mambo yajayo.

“Huwa sizungumzii yaliyopita, hapa tunaangalia yajayo,” Ten Hag aliiambia The Sun.

Al Nassr walifurahia kupata saini ya mchezaji huyo mwenye ufuasi mkubwa kwenye Instagram na inasemekana kuwa kumsaini kwao ni kama nyongeza kwa kampeni zao za kusaka kibali cha kuwa waandaaji wa mashindano ya kombe la dunia mwaka 2030.