Ronaldo alikuwa mbioni kujiunga Arsenal kabla ya Al Nassr kumnyakua, rafiki wake afichua

Kulingana na rafiki huku wa karibu wa Ronaldo, alikuwa tayari kusaini mkataba wa hadi mwisho wa msimu Arsenal lakini uongozi wa wanabunduki haukuwa tayari.

Muhtasari

• Morgan alielezea kwamba Arsenal ndio walidinda kuwasilisha ombi la kumpa mkataba wa hadi mwisho wa msimu, kitu ambacho Ronaldo alikuwa tayari kukubali.

Piers Morgan afichua jinsi Ronaldo alikuwa karibu kujiunga Arsenal
Piers Morgan afichua jinsi Ronaldo alikuwa karibu kujiunga Arsenal
Image: Goal// Twitter

Mwanahabari mwenye utata, shabiki wa Arsenal na ambaye ni rafiki wa karibu wa mchezaji maarufu kutoka Ureno, Christiano Ronaldo, Piers Morgan amefichua makubwa kuhusu mchezaji huyo mwaka jana kipindi mkataba wake ulivunjwa katika klabu ya Manchester United.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Morgan alikuwa anamjibu shabiki mmoja ambaye alikuwa anataka kujua aliko Ronaldo.

“Ronaldo yuko wapi Piers, yuko wapi?” Shabiki huyo aliuliza.

Kwa kumjibu, Morgan ambaye hajui kuficha siri alimwaga mtama kwenye kuku wengi akisema jinsi Ronaldo alikuwa karibu Zaidi kujiunga Arsenal kabla ya klabu ya Al Nassr kutoka Saudi Arabia kuingilia kati na kuibuka washindi katika mawindo ya mkataba wa Mreno huyo.

Morgan alielezea kwamba Arsenal ndio walidinda kuwasilisha ombi la kumpa mkataba wa hadi mwisho wa msimu, kitu ambacho Ronaldo alikuwa tayari kukubali.

Aliwasuta Arsenal kwamba walipoteza pakubwa kwa kutomsaini Ronaldo ambaye alikuwa tayari kujiunga nao na ndio maana wameshindwa kuendeleza moto wako katika mbio za ubingwa wa EPL msimu huu, huku sasa City ikiwa na nafasi kubwa ya kuchukua ubingwa huo kwa mara ya tatu mtawalia.

“Kejeli yote kwenu, lakini ikiwa tungemsajili Ronaldo alipoondoka Utd, hadi mwisho wa msimu - kama alivyokuwa na nia ya kufanya kwa taarifa yako - tungeshinda Ligi. Anajua jinsi ya kushinda mataji makubwa, na jinsi ya kufunga mabao muhimu wakati anahitajika,” Morgan alisema.

Madai ya Morgan yalikuja wakati Ronaldo anafurahia msimu mzuri wa kwanza akiwa na Al Nassr, akiwa tayari amefunga mabao 17 tangu ajiunge na wababe hao wa Saudia.

Ikumbukwe uhusiano wa Ronaldo na United uliingia doa kufuatia mahojiano makali na mwanahabari huyo ambapo mchezaji huyo alifichua mengi ya kukera kwa uongozi wa United kutoka kwa kocha hadi kwenye chumba cha kubadilisha nguo na mazoezini.