Mwisho wa kwisha: Christiano Ronaldo adokeza kustaafu kucheza soka mwaka 2025

Mshindi huyo mara tano wa tuzo mahiri ya Ballon d’Or, ambaye amewahi kucheza Manchester United, Real Madrid na Juventus, alianza kazi yake ya kulipwa zaidi ya miaka 18 iliyopita.

Muhtasari

• Mwaka jana, CR7 aliweka kikomo utawala wake wa malimwengu ya soka barani Ulaya baada ya mafanikio makubwa na kuondoka zake Saudi.

Christiano Ronaldo.
Christiano Ronaldo.
Image: Instagram

Nahodha wa muda mrefu wa Ureno, Cristiano Ronaldo anafikiria kustaafu soka wakati kandarasi yake ya sasa na klabu ya Al Nassr inayoshiriki Ligi ya Saudia inaisha mwaka 2025.

Fowadi huyo mwenye umri wa miaka 38 alikuwa akizungumza baada ya kuisaidia Al Nassr kupata ushindi wa 2-1 dhidi ya Damac katika mechi yao ya hivi punde ya Ligi ya Saudia Jumamosi, Oktoba 21.

Kulingana na Sportskeeda, Ronaldo alidokeza kuwa anaweza kufikiria kuachana na mchezo huo ambao umempa umaarufu atakapochunguza mwili wake ipasavyo mwishoni mwa mkataba wake wa sasa.

"Nitaendelea kucheza msimu huu na ujao. Kisha nitaangalia mwili wangu kuona kama naweza kuendelea au la. Mchezo ulikuwa mgumu hasa ulivyokuja baada ya michezo ya timu ya taifa na safari zilizofuata," Nyota wa Al Nassr alinukuliwa.

Mshindi huyo mara tano wa tuzo mahiri ya Ballon d’Or, ambaye amewahi kucheza Manchester United, Real Madrid na Juventus, alianza kazi yake ya kulipwa zaidi ya miaka 18 iliyopita baada ya kucheza kwa mara ya kwanza katika klabu ya Sporting CP ya Ureno mwaka 2002.

Mwaka jana, CR7 aliweka kikomo utawala wake wa malimwengu ya soka barani Ulaya baada ya mafanikio makubwa na kuondoka zake Saudi baada ya kile kilichosemekana ni kutofautiana na kocha wa Manchester United, Erik Ten Hag.

Nchini Saudi Arabia, msimu wa kwanza haukuwa rahisi kwake lakini msimu huu umemkubali mchezaji huyo ambaye licha ya umri wake kusonga, amewaongoza vijana kuwafunza soka uwanjani huku akitinga mabao kwa ustadi na starehe kama ambavyo amekuwa akifanya tangu akiwa tineja.