Nahodha wa Chelsea Reece James kuwa nje kwa angalau miezi 3 kufuatia jeraha la Hamstring

James katika misimu ya hivi karibuni amekuwa akisumbuliwa na jeraha na msuli wa paja na sasa imeripotiwa kwamba yuko tayari kutafuta ushauri na matibabu kutoka kwa mtaalamu wa tatizo hilo.

Muhtasari

• Baada ya uchunguzi wa kimatibabu na madaktari wa timu, imebainika kwamba alipata jeraha la misuli ya paja, kwa kimombo hamstring.

Reece James kuwa nje hadi Machi.
Reece James kuwa nje hadi Machi.
Image: CHELSEA

Ni pigo kwa timu ya Chelsea kwa mara nyingine tena baada ya nahodha wao Muingereza Reece James kuthibitishwa kupata jeraha ambalo huenda likamueka nje ya uwanja kwa angalau miezi miwili hadi mitatu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyoachiliwa na timu hiyo kupitia tovuti yao Jumanne mchana, Reece James alipata jeraha Jumapili wakati wa mpambano wao dhidi ya Everton ugani Goodson Park, mechi ambayo The Blues walipigwa mabao 2-0.

James alitolewa mchezoni kunako dakika ya 26 na nafasi yake kuchukuliwa na kinda Levi Colwill na sasa baada ya uchunguzi wa kimatibabu na madaktari wa timu, imebainika kwamba alipata jeraha la misuli ya paja, kwa kimombo hamstring.

Japo klabu hicho hakikutaja muda kamili ambao James anatarajiwa kuwa nje akijiuguza, wadadisi wa masuala ya spoti wanahisi huenda jeraha hilo likamfungia kutoshiriki mechi yoyote hadi mwishoni mwa Februari au mapema mwezi Machi mwakani.

“Nahodha Reece James amefanyiwa uchunguzi wa kimatibabu kufuatia kushindwa kwa mabao 2-0 Jumapili na Everton. Beki huyo alitolewa nje kipindi cha kwanza katika uwanja wa Goodison Park, na matokeo ya uchunguzi yamethibitisha jeraha la misuli ya paja. Reece sasa ataanza mpango wake wa ukarabati huko Cobham,” ripoti hiyo ilisoma kwa ukamilifu.

Mchezaji huyo beki wa kulia amekuwa akisumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara na sasa ripota wa Evening Standard anayeshughulikia taarifa za Chelsea, Nizaar Kinsella amethibitisha kwamba James huenda akalazimika kutafuta matibabu na ushauri kutoka kwa mtaalamu wa jeraha la msuli wa paja katika azma ya kumaliza tatizo la jeraha hilo ambalo limekuwa likimuandama mara kwa mara.

James sasa anaingia katika orodha ndefu ya majeruhi wa Cheslea wakiwemo mlinda lango Robert Sanchez, mabeki Weslay Fofana, Malo Gusto, Marc Cucurella na Ben Chilwell, viungo wa kati Ugochukwu, Chukwuemeke, Romeo Lavia, Madueke na mshambuliaji Christopher Nkuku.