Christiano Ronaldo amtumia Mbappe ujumbe baada ya uhamisho wa Real Madrid

Ronaldo amefurahishwa na Kylian Mbappe kujiunga na Real Madrid huku akisema kuwa ni wakati wa kumtazama akicheza ugani Santiago Bernabeu.

Muhtasari

•Christiano Ronaldo amefurahishwa na uhamisho wa Mbappe kuelekea Real Madrid akitaja kuwa yupo tayari kumuona Mbappe akifaulu kwenye ligi ya La Liga.

•Uhamisho wa Kylian Mbappe kwenda Real Madrid ulithibitishwa Jumatatu wakati akisaini mkataba wa miaka mitano

Kylian Mbappe pamoja na Christiano Ronaldo
Image: KMbappe/X

Cristiano Ronaldo amefurahi kumuona Kylian Mbappe katika klabu ya Real Madrid baada ya nyota huyo wa Ufaransa kuhamia Bernabeu kutoka PSG kuthibitishwa.

Kylian Mbappe mwenye umri wa miaka 25 amejiunga na Los Blancos kwa mkataba wa miaka mitano. Nyota wa kimataifa wa Ureno na Al-Nassr Ronaldo alikuwa miongoni mwa waliotuma salamu zao za heri kwa Mbappe.

 Christiano amechezea Real Madrid  miaka tisa akishinda mataji muhimu kama vile kombe la UCL na yale ya klabu bingwa duniani.Kylian Mbappe alionekana kuvutiwa na mshambulizi huyo wa Ureno akiwa anachezea Monaco.

"Ndoto imetimia, nina furaha sana na ninajivunia kujiunga na klabu ya ndoto yangu @realmadrid," Mbappe alisema kwenye mtandao wa kijamii.

"Hakuna anayeweza kuelewa jinsi ninavyofurahishwa sasa hivi... Hala Madrid!" Mbappe aliandika kwenye ukurasa wake wa X baada ya uhamisho kukamilika.

Ujumbe huo uliambatana na uteuzi wa picha zilizomuonyesha Mbappe akiwa katika kumbukumbu za Real Madrid.

Katika moja ya picha hizo, Mbappe alionekana akikutana na Ronaldo ndani ya vituo vya Les Merengues.Kylian Mbappe amekuwa akimtaja Christiano Ronaldo kama mfano miongoni wa wachezaji anaowaiga tangu utotoni.

Christiano alitoa pongezi kwa usajili wa hivi punde zaidi wa Real Madrid. Inaonekana mkongwe huyo anatamani kuona maisha ya Mbappe yakiendelea kwenye ligi ya La Liga

"Zamu yangu ya kukutazama ukicheza .... Nimefurahi kukuona Bernabéu. #HalaMadrid" Ronaldo alichapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram.