Kevin De Bruyne asema yuko tayari kwa uwezekano wa kuhamia ligi ya Saudi

Kevin De Bruyne ameweka wazi nia yake ya kuhamia kwenye ligi ya Saudi huku akiwa anasalia na mkataba wa mwaka mmoja Manchester City.

Muhtasari

•Kevin De Bruyne amefunguka kuhusu kuhamia ligi ya Saudi iwapo ofa yoyote itatokea.

•Mchezaji huyo amedai kuwa cha msingi kwake ni pesa hasa ikizingatiwa kuwa miaka yake imeenda na maisha yake ya baadaye ni ya muhimu mno.

Kevin De Bruyne
Image: X

Kevin De Bruyne amefunguka kuhusu uwezekano wa kuhamia ligi ya Saudi iwapo ofa yoyote itatokea hivi karibuni ama mwishoni mwa kandarasi yake.

Kiungo wa kati wa Manchester City Kevin De Bruyne amesema kuwa yupo tayari kuhamia kwenye ligi ya Saudi iwapo ofa yoyote itatokea.Kwenye mahojiano na jarida la Hlsport,De Bruyne amedokeza kuwa katika umri wake lazima mtu awe na uwazi na awe na maoni ya baadaye hasa kama mchezaji ambaye miaka imeenda.

"Unazungumza juu ya pesa nyingi sana katika kile ambacho kinaweza kuwa mwisho wa kazi yangu.Wakati mwingine unapaswa kufikiria kuhusu hilo.Nikicheza huko kwa miaka miwili,nitaweza kupata kiasi cha ajabu..' De Bruyne alisema.

Mchezaji huyo aidha amefichua kuwa amekuwa akicheza mpira kwa zaidi ya miaka 15 na huenda akijumulisha kiwango cha fedha alichopokea kwa hizo miaka kisifikie kile cha Saudi kwa miaka miwili.

"Kabla ya hapo nililazimika kucheza  mpira wa miguu kwa miaka 15.Huenda hata nisifikie kiasi hicho..unafaa kufikiria ni nini kinachowezakumaanisha baadaye..."

 

Kwa sasa De Bruyne amesalia na mkataba wa mwaka mmoja,Manchester City.Mchezaji huyo amecheza mechi 382 kwa miaka tisa tangu ajiunge na Manchester City,huku akishinda mataji sita ya ligi kuu ya Primia na kombe la klabu bingwa Ulaya.

Ligi kuu ya Saudi ilianza  kupata umaarufu baada ya Christiano Ronaldo kujiunga na Al-Nassr mwaka  wa 2023. Wachezaji wengi wababe wamejiunga na vilabu vya Saudi kama vile  Karim Benzema,Ngolo Kante,Fabinho,Jota,Neymar na wengineo.