Thiago Motta ateuliwa na Juventus kama kocha mpya

Allegri alibanduliwa na Juventus kutokana na utovu wa nidhamu katika mechi dhidi ya Atalanta

Muhtasari

•"Nina furaha mpwitompwito kushika hatamu mpya kwenye klabu bingwa ya Juventus," alisema Motta.

•Allegri alibanduliwa na klabu hiyo kufuatia utovu wa nidhamu dhidi ya Atalanta. 

Kocha mpya wa Juventus, Thiago Motta
Image: HISANI

Mabingwa wa mara 36  wa  Ligi Kuu ya Italia Serie A, Juventus, wamemteua Thiago Motta kuwa kocha wao mpya baada ya kumtimua Massimiliano Allegri mwezi uliopita kufuatia utovu wa nidhamu kwenye mechi dhidi ya Atalanta.

"Ni rasmi, kocha mgeni wa Juventus atakuwa Thiago Motta. Raia huyo wa asili ya Italia na Brazil ametia sahihi kwenye mkataba wake na Juventus mpaka mnamo Juni 30, 2027," klabu iliandikisha ujumbe huo.

Motta mwenye umri wa miaka 41 amekuwa akihudumu kama kocha wa timu ya Bologna.

"Nina furaha mpwitompwito kushika hatamu mpya kwenye klabu bingwa ya Juventus," alisema Motta.

Kulingana na vyombo vya habari vya Italia,Motta atakuwa akipokea mshahara wa takriban euro milioni 3.5 kwa mwaka.

Mchezaji huyo wa zamani wa kimataifa wa Italia alikuwa kwenye kikosi kilichomaliza katika nafasi ya pili katika michuano ya Ulaya ya 2012.

Vilevile, alikuwa bingwa mara tano na kikosi cha Ufaransa cha PSG na pia kuchezea timu za Barcelona na Inter Milan.

Klabu ya Juventus itakuwa ya nne kwake kuhudumu kama kocha. Awali, alihudumu kama kocha wa Genoa mnamo 2019 ambapo alikaa kwa miezi mitatu kabla ya kupigwa kalamu kufuatia rekodi ya kushinda mechi moja kwa kumi zilizochezwa.

Fauka ya hayo, alihudumu katika klabu ya La Spezia (2021/22) kisha akaenda Bologna kabla ya kuteuliwa kuwa meneja waJuve.

Juventus walimaliza katika nafasi ya tatu Serie A wakiwa na alama 23 nyuma ya mabingwa wa ligi wa msimu huo, Inter Milan.

Allegri alibanduliwa na klabu hiyo kufuatia utovu wa nidhamu dhidi ya Atalanta. Si hayo tu, bali alielekea kuwakashifu wasimamizi wa mechi hiyo kabla ya kumtishia mhariri mkuu wa gazeti la Tuttosport.

Utovu huu wa nidhamu na tabia hii ilichochea uchunguzi kuzuka kutoka kwa Mamlaka ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka la Italia.

Allegri alishinda mataji 12 ikiwemo matano ya Serie A na pia alifika kwenye fainali mbili za ubingwa wa Ulaya akiwa meneja wa Juve.