Harambee Stars yapata ushindi mkubwa, yaadhibu Seychelles mabao 5-0

Kenya sasa imapanda hadi nafasi ya tatu katika kundi 'F', na kujikusanyia pointi tatu muhimu.

Muhtasari

• Nahodha Michael Olunga aliongoza kwa mfano alipofunga mabao mawili chini ya dakika 10 za mwanzo, na hivyo kibarua dhidi ya wapinzani wao kuwa kigumu.

• Benson Omalla aliyetokea benchi alifunga bao  la tano ambalo ni bao lake la kwanza kwa timu hiyo kunako dakika ya 73.

Image: HISANI

Harambee Stars ilifanya kazi ya ziada baada ya ushindi wao wa 5-0 dhidi ya Seychelles mnamo Jumatatu katika mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia la 2026 kwenye Uwanja wa Stade Felix Houphouet-Boigny mjini Abidjan, Ivory Coast.

Awali, vijana hao wa Kocha  Engin Firat walikuwa wamepoteza mechi yao ya ufunguzi kwa mabao 2-1 dhidi ya Gabon.

Nahodha Michael Olunga aliongoza kwa mfano alipofunga mabao mawili chini ya dakika 10 za mwanzo, na hivyo kibarua dhidi ya wapinzani wao kuwa rahisi.

Masud Juma alifunga bao kabla ya muda wa mapumziko na kuwa mbele kwa mabao 3-0.

Baada ya mapumziko, Rooney Onyango aliingia wavuni huku bao lake la dakika ya 62 likizidisha makali ya Kenya.

Benson Omalla aliyetokea benchi alifunga bao  la tano ambalo ni bao lake la kwanza kwa timu hiyo kunako dakika ya 73.

Kenya sasa imapanda hadi nafasi ya tatu katika kundi 'F', na kujikusanyia pointi tatu muhimu katika harakati zao za kufuzu kwa Kombe la Dunia la 2026 litakaloandaliwa na Marekani, Mexico na Canada.

Mkufunzi, Firat alifanya mabadiliko mawili ambayo yalichangia kwa vijana wake kupata ushindi.

Kikosi kilichosalia kilibaki bila kubadilika, huku Anthony Akumu na Richard Odada wakiunda ushirikiano wa safu ya katiwakati Masud Juma na Michael Olunga wakipambana kusaka bao.

Dennis Ng’ang’a alishirikiana na Johnstone Omurwa katika safu ya ulinzi, huku Rooney Onyango akiweka nafasi yake kwenye kikosi cha kwanza kwa mechi ya tatu mfululizo.