Mwanamke atiwa mbaroni kwa kuchangia mauwaji ya mumewe

Polisi kaunti ya Kisii wanamzuilia mwanamke kutoka kijiji cha Chirenge anayesemekana aliwalipa wahuni wamsaidie kumuua mumewe mwenye umri wa miaka 42.

Mwili wa Nelson Nyamai ulipatikana na nduguye James Nyamo ambaye alipokea simu kutoka kwa mtu asiyemfahamu akimuarifu kuwa Nelson alikuwa ameuawa.

James aliiambia Citizen Digital kuwa mwili wa marehemu ulikuwa na majeraha ya kukatwa shingoni na kichwani.

James pia alidokeza kwamba alipomuuliza mkewe marehemu, alikiri kuhusika katika mauaji hayo na hata kumuonesha vifaa vilivyotumika kutekeleza uhayawani huo.

Mwili wa marehemu umelazwa katika makafani ya hospitali ya rufaa ya Kisii huku mshukiwa naye akizuiliwa katika kituo cha polisi cha Kiogoro.

Polisi walisema wangali wanachunguza kiini cha mauaji hayo huku wahusika wengine wakiendelea kusakwa.