PATANISHO: Sipendi tabia za mume wangu za kuskiza watu!

Charles Nyacheo. 30, aliomba apatanishwe na mkewe, bi Sophie, 27, baada ya wawili hao kukosana mwezi uliopita kwa sababu ya mambo ya kifamilia akidai kuwa wawili hao hawaaminiani.

"Mimi hufanya kazi usiku na nikitoka marafiki huniambia kuwa mke wangu hayuko kwa nyumba na unapata kuwa tunakorofishana na kuna wakati nilimpiga kwa sababu ya hasira. Hapo alienda nyumbani na baadaye nikaskia anaishi na shemeji yangu." Alisema.

Charles anasema juhudi zake za kumbembeleza mkewe hazijafua dafu na kila anapomwambia warudiane mkewe humuarifu kuwa anapaswa kuishi na wale marafiki waliokuwa wanampa mawaidha.

Wawili hawa wamekuwa kwa ndoa ya miaka minane na wamejaliwa na watoto watatu.

"Ni nini umeona kizuri tena kwangu ukaamua kunirudia? Tulijuana nawe kitambo nikiwa shuleni na sielewi mbona uliskiza maneno ya watu." Sophie alisema akimkemea mumewe.

Aliongeza akisema hapendi tabia yake ya kuskiza mambo ya watu na kama atarudiana naye hatarajii afanye hilo tena na yuko tayari kuishi kivyake alee watoto wao.

Wawili hao walisameheana na kuahidiana kupendana na kubadilisha tabia, haswa bwana Charles.