Rais Yoweri Museveni aanza matembezi ya siku 6 jangwani, sababu zatolewa

Rais wa Uganda Yoweri Museveni ameanza matembezi ya siku sita jangwani, kama sehemu ya kumbukumbu ya jinsi vikosi vyake vilivyopambamba mwaka 1986 kunyakua madaraka mikononi mwa Idi Amin na Milton Obote.

Wapinzani wake wamekosoa matembezi hayo wakidai kuwa na mpango wa kujipatia umaarufu kabla ya uchaguzi mkuu mwaka ujao, ambapo Bw. Museveni anatarajiwa kugombea urais kwa muhula wa sita.

Anakabiliwa na upinzani kutoka kwa msanii wa zamani wa muziki na mwanasiasa Bobi Wine, ambaye amejitangaza kama mkombozi wa maskini. 

Mkusanyiko wa habari humu nchini

Watu watatu waliaga dunia jana katika ajali iliyotokea Ugunja katika barabara ya Kisumu kwenda Busia. Kamanda wa polisi wa Siaya Francis Kooli amesema mtu mmoja alijeruhiwa vibaya. Ajali hiyo iliyotokea wakati dereva wa basi moja lililokuwa likienda Kisumu alipopoteza mwelekeo na kuligonga gari dogo.

 Usalama umeimarishwa huko lamu kufuatia shambulizi dhidi ya basi moja na washukiwa wa al shabab. Msemaji wa serikali Cyrus Oguna amesema maafisa wa usalama wapo katika hali ya tahadhari kukabiliana na jaribio lolote la mashambulizi.

Chuo kikuu cha Nairobi kina naibu mhadhiri mkuu mpya baada ya Profesa Stephen Kiama kupewa barua ya uteuzi. Jina lake lilikuwa miongoni mwa ya watu wengine watatu yaliowasilishwa kwa waziri wa elimu George Magoha. Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kuidhinisha rasmi uteuzi huo hapo kesho.

Serikali imepata lita 3000 za kemikali ya kukabiliana na nzige ambao wamevamia sehemu za kaskazini mwa nchi. Msemaji wa serikali Cyrus Oguna amesema watatumia ndege kuinyunyiza kemikali hiyo katika sehemu zilizovamiwa na wadudu hao wa kuruka.