Sakata: Afisa wa KPA achunguzwa kuhusu malipo ya shilingi milioni 90

HAJJI
HAJJI
Afisa mmoja wa cheo cha juu katika Halmashauri ya Bandari nchini ambaye ni mshukiwa mkuu katika sakata tofauti ya shilingi bilioni 2.7 alipokea shilingi milioni 90 katika njia tatanishi kutoka kwa shirika hilo kulingana na ripoti ya ujasusi.

Uchunguzi huo mpya wa tume ya maadili na kupambana na ufisadi nchini EACC umeshirikisha pia shirika la Telkom Kenya ambalo akaunti zake katika Benki ya Standard Chartered zimefungwa kwa muda wa miezi sita.

Stakabadhi za mahakama ambazo zimetufikia zaonyesha kuwa Anthony Muhanji, afisa wa cheo cha juu, anadaiwa kupokea shilingi milioni 90 kupitia kampuni yake, Mukitek Investment Ltd.

Tume ya kupambana na ufisadi inasema kwamba malipo hayo kutoka KPA huenda ni ufisadi kwa sababu hakuma stakabadhi za kuonyesha uhalali wa malipo hayo.

Maswali yameibuka kuhusu sababu ya shirika la kitaifa kulipa kampuni inayomilikiwa na mmoja wa wafanyikazi wake katika hali ambayo inaonekana kuwa matumizi mabaya ya afisi.

"Kuna sababu za kutosha kwamba washukiwa walipokea pesa kutoka Halmashauri ya bandari nchini kupitia njia za ufisadi kinyume na sheria za kukabiliana na ufisadi,” stakabadhi za EACC mahakamani zilieleza.

Maafisa wa uchunguzi wa tume ya EACC na DCI wamepiga kambi katika afisi za KPA mjini Mombasa kwa mwezi mmoja sasa. Idara ya DCI tayari imekamilisha uchunguzi katika sakata tofauti ya shilingi bilioni 2.7 bandarini na kupendekeza kushtakiwa kwa maafisa kadhaa wa ngazi za juu wa shirika hilo akiwemo Muhanji.  Wengine ni Meneja Mkurugenzi Daniel Manduku, Meneja mkuu anayesimamia oparesheni William Rutto na afisa mkuu wa utendaji Bernard Nyobange.

Katika kesi moja, idara ya DCI iligundua kwamba shilingi bilioni 3 zilizokuwa zimetengwa na kuidhinishwa kwa ununuzi wa ardhi ya ujenzi wa bandari ya nchi kavu mjini Nairobi zilizobadilishwa na kutumiwa kwa ukarabati wa eneo la kuweka mizigo la Makongeni kwa kima cha shilingi milioni 500. Bilioni mbili zilitumiwa kuondoa uchafu na kuchimba Bandari ya Mombasa huku milioni 500 pekee zikiashwa kwa ujenzi wa bandari ya nchi kavu.

Stakabadhi za EACC zaonyesha kwamba Muhanji alitoa shilingi milioni 5.5 ambazo zilikuwa sehemu ya pesa zilizolipwa kwa kampuni yake kwa awamu tatu. Kisha alihamisha shilingi milioni 50 hadi akaunti ya shirika la Telkom, kwa ununuzi wa nyumba inayomilikiwa na shirika hilo katika mtaa wa Kileleshwa mjini Nairobi.

Shirika la Telkom lilipoulizwa kwanini lilipokea pesa kutoka kwa kampuni ya Mukitet Investment Ltd, shirika hilo lilisema kamba pesa hizo zilitoka kwa kampuni tofauti, Stone Contractors Ltd kwa ununzi wa nyumba. Hata hivyo, uchunguzi wa EACC ulifichua kwamba Muhanji pia anauhusiano na Stone Contractors Ltd.

Baada ya kufuata mkondo wa pesa hizo, EACC siku ya Ijumaa ilipata agizo la makama kufunga kwa muda akaunti za shirika la Telkom Kenya. Hatua hiyo inalenga kuzuia shirika hilo la mawasiliano kutumia pesa hizo huku tume hiyo ikilenga kuwasilisha ombi la kurejesha pesa hizo kutoka kwa Muhanji.