Vijana kunufaika na mradi wa takriban shilingi bilioni 15

Serikali inalenga kubuni nafasi za ajira kwa zaidi ya vijana elfu 50 chini ya mpango wa kupiga jeki ajira kwa vijana  (Kenya Youth Employment and Opportunities Project - KYEOP).

Katibu mwandamizi katika wizara ya ICT Nadia Ahmed Abdalla siku ya Jumatano alitoa wito kwa vijana kutumia nafasi hii vyema ili kunufaika kutokana mradi huu wa shilingi bilioni 15.

Akizungumza katika hafla ya kukagua maandalizi ya walimu wanaongoza mradi huu Nadia alisema kwamba mradi huu utanufaisha vijana kutoka kaunti teule 17.

Mafunzo hayo yalisitishwa kutokana na janga la corona lakini serikali imeanza mikakati ya kujiandaa kurejelea mafunzo hayo huku maambukizi ya Covid-19 yakionekana kupungua.

Katibu huyo mwandamizi alipongeza mradi wa KYEOP kwa kuwapa vijana ujuzi unaohitajika katika kupata ajira, kuanizisha biashara na hata kuajiri watu wengine.

"Nimekuwa nyanjani na nimeona kile KYEOP imefanyia vijana," Nadia alisema.

Aliongeza kuwa, "Lazima tukumbuke Kenya ni mimi na wewe...yafaa tuelewe kwamba kuna mengi tunayoweza kufanya kutokana na fursa tulizopewa".

Wakati wa hafla hiyo, Nadia pia alizuru maonyesho mbali mbali ya ushonaji, mitindo na ubunifu na sanaa.

Awamu ya nne ya mafunzo hayo ilisitishwa mwezi Machi kutokana janga la Covid-19.

Mradi wa KYEOP ni wa shilingi bilioni 15 na unafadhiliwa na Benki ya Dunia na unalenga kuwapa ujuzi muhimu vijana wa kati ya miaka 18- 29 wa kiwango cha kidato cha nne  kwenda chini.

Mradi huyo unatakelezwa katika kaunti 17 zikiwemo: Mombasa, Kilifi, Nairobi, Nakuru, Kiambu, Nyandarua, Mandera, Turkana, Wajir, Bungoma, Kakamega, Kisumu, Kisii, Machakos, Kitui na Migori.

Shughuli za kuchagua kaunti zinazoshiriki ilizingatia vigezo kama vile; idadi ya watu, viwango vya umaskini, mchanganyiko wa watu wa mijini na mashambani miongoni mwa vigezo vingine.

Kufikia sasa jumla ya vijana, 32,124 wamepokea mafunzo hayo na kupata ujuzi kutoka sekta mbali mbali huku asilimia 75 wakipata ajira kulingana na takwimu zilizotolewa.