Mbusii afichua wakati alipoanza kukuza rasta zake

Mwendani wake Lion pia alieleza maoni yake kuhusu warasta

Muhtasari

• Mbusii alisema  alianza kuzilea mwaka wa 2006 kisha baada ya miaka miwili akanyolewa na maafisa wa usalama.

•Lion alifichua kuwa mtoto wake ambaye anasoma katika shule ya msingi amekuza dreadlocks.

Watangazaji Lion na Mbusii

Mtangazaji wa kipindi cha Mbusii na Lion Teke Teke kwenye Radio Jambo Daniel Githinji Mwangi almaarufu Mbusiii amefunguka kuhusu rasta zake.

Katika mahojiano yake na mwandishi Caroline Mbusa, Mbusii alisimulia kinagaubaga kuhusu safari ya kukuza nywele zake ndefu.

Alisema kwamba  alianza kuzilea mwaka wa 2006 kisha baada ya miaka miwili akanyolewa na maafisa wa usalama.

"Serikali walinitandika viboko, wakaziakata zote na panga, nikatulia mwaka mmoja ndipo nikaanza kulea hizi ambazo niko nazo," alisema.

Mtangazaji mwenzake Cyrus Afune almaarufu Lion pia alitoa maoni yake kuhusu watu kuweka nywele ndefu (rasta).

Alieleza kuwa anaunga mkono mtindo huo wa nywele kwani kulingana naye, 'warasta' ni watu ambao wanapenda mambo ya kweli.

"Dreadlocks ni zetu na tuko hapa kuzikubali na kuzithamini. Si lazima kuwa na dreadi ili kuwa rasta," Lion alisema.

Alifichua kuwa mtoto wake ambaye anasoma katika shule ya msingi amekuza dreadlocks baada ya serikali kuukubali mtindo huo wa nywele.

Lion alisema kuwa warasta ni watu wazuri na ni watu wa kawaida, kinyume na wanavyodhani wengine kuwa ni watu wabaya.

"Msiwaone watu wenye dready kama wakora,ama kuwa ni watu wanaovuta bangi. Bangi ni mihadarati ambayo huvutwa hata na watu ambao hawana mtindo huo wa nywele," Mbusii alikubaliana na mwenzake.