Patanisho: Mwanadada agura ndoa ya mwaka mmoja baada ya mumewe kumpiga na kumvunjia simu

Muhtasari

•Caroline alisema ndoa yao ya mwaka mmoja tu tayari imeanza kuwa na misukosuko kwani mumewe ambaye ni mwendesha bodaboda amegeuka kuwa mkali kwake na amekuwa akimpiga.

•Caroline alisema aliamua kuenda kwao ili kupumzisha akili kufuatia ghadhabu aliyopata kutokana na kichapo cha mumewe.

•Kea alipopigiwa simu alikanusha madai ya kumpiga mkewe huku akidai Caroline ndiye alifanya maamuzi ya kuondoka.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho mwanadada aliyejitambulisha kama Caroline Shikuku (21) alituma ujumbe akiomba kusaidiwa kurudiana na mume wake Kea (25) 

Caroline alisema ndoa yao ya mwaka mmoja tu tayari imeanza kuwa na misukosuko kwani mumewe ambaye ni mwendesha bodaboda amegeuka kuwa mkali kwake na amekuwa akimpiga.

Alisema wakati ambapo alifanya maamuzi ya kugura ndoa mumewe alifika nyumbani jioni akampiga. Baada ya kichapo kile Caroline alizungumza na baba mkwe ambaye alimhakikishia kwamba angeongea na mwanawe ila siku iliyofuata akamshambulia tena.

"Tulipatana naye mahali tulikuwa tunatazama mpira tukajuana kisha akanioa. Yeye ni mtu wa bodaboda. Huwa anakuja anapata nimefanya kila kitu. Sijui ni nini huwa amekunywa, ama ni pombe. Huwa anaanza tu kunifanyia madharau . Nikimwambia eti sijafanya kitu anaanza tu kunipapiga bila sababu. Alinipiga mpaka akanipasulia simu. Sijui kwa nini, ni kama alisikia mambo ya nje. Alikuja akanipiga nikaambia hata babake akasema atamuongelesha, kesho yake akaenda huko akarudi akanipiga mimi nikaenda nyumbani" Caroline alisema.

Caroline alisema aliamua kuenda kwao ili kupumzisha akili kufuatia ghadhabu aliyopata kutokana na kichapo cha mumewe.

Hata hivyo alisema yuko tayari kumsamehe mumewe na kurudiana naye kwa kuwa ana mapenzi makubwa sana kwake.

Kea alipopigiwa simu alikanusha madai ya kumpiga mkewe huku akidai Caroline ndiye alifanya maamuzi ya kuondoka.

Alisema ako tayari warudiane na kumuomba mkewe arudi kwake. Caroline hata hivyo alimueleza ni sharti kwanza apige hatua ya kumwendea kwao ili wasuluhishe mzozo pamoja na wazazi.

"Mimi sikumpiga, ni uongo tu. Kama anasema nilimchapa na mimi najua sikumchapa, anisamehe basi. Ni kisirani tu cha watu kwa boma. Naomba arudi basi. Nitaenda kwao Jumapili" Kea alisema.

Wawili hao walikubaliana kurudiana baada ya Kea kuenda kwa kina Carol na kusuluhisha mzozo wao.

Je, una ushauri upi kwa wanandoa hao?