• “Mtoto alikuwa ashakuwa mkubwa, mwaka mmoja na nusu. Aliendesha nikampeleka hospitali akadungwa sindano na hivyo ndivyo aliaga" alisema.
Katika kipindi cha Patanisho kwenye Gidi na Ghost asubuhi katika stesheni ya Radio Jambo, mrembo kwa jina Valentine mwenye umri wa miaka 26 aliomba kupatanishwa na bwanake kwa jina Joseph Oginga mwenye miaka 32.
Valentine alisema walikaa na mume wake kwenye ndoa kwa kipindi cha miaka 2 na baada ya kupata mtoto, alifikisha umri wa mwaka mmoja na nusu na akaaga baada ya kuharisha kwa wiki moja.
Tangu mwezi Aprili mwaka jana mpaka sasa hivi alipoenda kwao mume wake hajapata kumtafuta warudiane na alitaka kujua hatima ya ndoa yake kupitia Patanisho.
“Tulikuwa tunavurugana kiasi lakini baada ya kupata mtoto na bahati mbaya akaaga, tulimzika siku iliyofuata familia yake wakaanza kunionyesha madharau. Nikaenda kwa bwanangu naye akaniambia nimpe muda. Mtoto tulimzika kwa kina mume wangu.”
“Mtoto alikuwa ashakuwa mkubwa, mwaka mmoja na nusu. Aliendesha nikampeleka hospitali akadungwa sindano na hivyo ndivyo aliaga. Aliendesha kwa wiki moja na madakttari walituambia tulikuwa tumempa dawa zingine nyumbani zikachanganyikana na za hospitali,” aliongeza.
Bwana Joseph alipopigiwa simu, alisema kwamba hana tatizo na mke wake kwani mara ya mwisho wakizungumza alimtaka kwenda nyumbani kwao hali ya kuwa yeye [Joseph] yuko Nairobi.
“Mimi naona sina shida na yeye lakini labda aende kwa wazazi, kuna wakati aliniambia aende kwa wazazi tayari ako kwao, mimi niko Nairobi. Mimi sina shida na yeye, atoke tu aende kwa wazazi wangu Kisumu. Hatuwzi kuwa tunaishi Nairobi na mke anaona nimeshamjengea nyumba…”
Joseph alipozungumza na Valentine, alimsisitizia kwamba aende nyumbani kwao Kisumu kwa sababu kuna nyumba yake huko.
Hata hivyo, Valentine alibisha wazo hilo la kwenda nyumbani kwa kina mume akisema kwamba yeye anataka kuishi karibu na mumewe na kama ni kwenda nyumbani itakuwa ni mara moja moja tu kuwasalimia wazazi.
“Wewe unataka niende nikae huko peke yangu na wewe unakaa peke yako Nairobi kwa nini?” Valentine alimuuliza.