Mwanadada atoroka baada ya mumewe kugundua anatoka kimapenzi na deacon wa kanisa lao

Wanjala aligundua kuwa aliyekuwa amemtumia mkewe meseji ya kimapenzi ni shemaji katika kanisa lao.

Muhtasari

•Wanjala alifichua kuwa ndoa yake ilisambaratika baada ya kugundua kuwa mkewe alikuwa akitoka nje ya ndoa.

•Baada ya Wanjala kufuatilia zaidi shemasi wa kanisa lao alikiri kuwa alikuwa akitoka kimapenzi na mke wake.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Zakayo Wanjala alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Nekesa ambaye alitengana naye kufuatia ugomvi wa kinyumbani.

Wanjala alifichua kuwa ndoa yake ilisambaratika baada ya kugundua kuwa mkewe alikuwa akitoka nje ya ndoa.

"Nilikuwa Homabay. Nilikuwa nikikuja mwisho wa mwezi. Siku moja nilikuja saa kumi na moja asubuhi. Nilichukua simu yake nikaona mwanaume akiwa amemtumia meseji iliyosoma 'Irene sitawahi kusahau na sitawahi kutafuta mtu mwingine'.." alisimulia.

Baada ya kusoma meseji ile Wanjala alimuamsha mkewe na kumuuliza kuhusu aliyekuwa amemtuma lakini hakupata jibu.

"Nilimuamsha polepole. Alipoamka nikamuonyesha meseji hiyo akashtuka. Nilipomuuliza akanyamaza," alisema.

Wanjala alisema alichunguza na kugundua kuwa mwanaume aliyekuwa amemtumia mkewe meseji ya kimapenzi ni shemaji katika kanisa lao. Alisema kuwa baada ya kufuatilia zaidi shemasi huyo alikiri kuwa alikuwa akitoka kimapenzi na mke wake.

"Alienda kwao. Nimekuwa nikimpigia anasema atakuja lakini hakuji," alisema.

Nekesa aligura ndoa yake pamoja na watoto wao wawili.

Wanjala alisema licha ya mkewe kutoka nje ya ndoa bado upendo wake kwake upo na anataka warudiane. 

Juhudi za Gidi kuwapatanisha wawili hao hazikufua dafu kwani Nekesa hakupatikana kwenye simu.