ALIACHWA NA FADHAA KUBWA

Mtangazaji Shiksha Arora asimulia aliyoyapitia mikononi mwa wezi waliomuibia katika tukio la kufadhaisha

Baada ya kutangaza kurudi kwake kwenye runinga asubuhi ya Jumatatu, jioni hiyo Arora alijipata mikononi mwa wezi watatu ambao walimuibia, wakajaribu kumuibia na kumuacha na fadhaa

Muhtasari

•Juni 21, 2021 itabaki kuwa siku ya kukumbuka maishani mwa malaika wa utangazaji, Shiksha Arora. Arora ataikumbuka siku hiyo kwa jambo nzuri lililomtendekea na jambo lingine la kuogofya.

•Kutokana na tukio hilo, Arora amewashauri wenye magari kuwa wasifungue madirisha yao wakiwa kwenye mzunguko wa Globe kwani wezi wale wanafanya uvamizi wakiwa wamejipanga kama timu.

Shiksha Arora
Shiksha Arora
Image: Hisani

Juni 21, 2021 itabaki kuwa siku ya kukumbuka maishani mwa malaika wa utangazaji, Shiksha Arora. Arora ataikumbuka siku hiyo kwa jambo nzuri lililomtendekea na jambo lingine la kuogofya.

Baada ya kutangaza kurudi kwake kwenye runinga asubuhi ya Jumatatu, jioni hiyo Arora alijipata mikononi mwa wezi watatu ambao walimuibia na kumyonga.

Kupitia mtandao wa Twitter, Arora alisimulia masaibu yaliyompata mida ya saa kumi na moja unusu alipokuwa katika  mzunguko wa Globe.

"Jana mida ya saa kumi na moja na dakika ishirini niliibiwa maeneo ya Globe. Jamaa mmoja aligonga kioo cha upande cha gari langu na kukipindua nyuma. Nilipokuwa nafungua dirisha ili kutengeneza kioo, jamaa wa pili akaanza kugonga dirisha la mbele upande wa abiria kwa nguvu.

Nilipokuwa naangalia upande wa kushoto, jamaa wa tatu akaingiza mkono wake ndani ya gari na kufungua, akaingia kwenye kiti cha nyuma na kukaa. Akachukua pochi langu na kuagiza simu yangu." Arora alisimulia.

"Kwa wakati huo nilikuwa nimeshtuka na singeweza kusema lolote. Jamaa yule akaitisha simu kwa mara nyingine, akafikia shingo langu na kuanza kujaribu kuninyonga.

Alipokuwa  anajaribu kuninyonga, nilijaribu kabisa  kupumua ili nipate hewa. Nikaanza kupiga honi ili kuvutia watu nikitumai kuwa wangekuja kunisaidia. Watu wakaanza kutoka ndani ya magari yao na hapo wezi wale wakatoroka" Arora aliendelea kusimulia

Alisema kuwa wezi hao walitoweka na pochi lake na kumuacha akiwa amefadhaika

Kutokana na tukio hilo, Arora amewashauri wenye magari kuwa wasifungue madirisha yao wakiwa kwenye mzunguko wa Globe kwani wezi wale wanafanya uvamizi wakiwa wamejipanga kama timu.

Hata hivyo, ameeleza kuwa hakuumia ila alichwa fadhaa kubwa.