Shukran Wakenya! Lolani Kalu atumia mchango wa Wakenya kufungua studio

Aliyekuwa mwanahabari wa NTV , Lolani Kalu sasa ameweza kujikimu tena

Muhtasari

•Masaibu yake yaliangaziwa kwenye mtandao wa Twitter na akaalikwa kwa mahojiano na Jalang'o ambapo aliomba mashabiki kumsaidia na kiwango chochote cha pesa ambacho wangeweza.

•Kwa sasa Kalu ameweza kujikimu tena na amefungua studio ya kurekodi muziki ambapo anasaidia wengine kurekodi.

Lolani Kalu akiwa kwenye studio yake
Lolani Kalu akiwa kwenye studio yake
Image: Hisani

Habari na Elizabeth Ngigi

Aliyekuwa mwanahabari wa NTV, Lolani Kalu amewashukuru Wakenya kwa kumsaidia wakati alihitaji msaada mwaka uliopita.

Masaibu yake yaliangaziwa kwenye mtandao wa Twitter na akaalikwa kwa mahojiano na Jalang'o ambapo aliomba mashabiki kumsaidia na kiwango chochote cha pesa ambacho wangeweza.

"Tunapoendelea, mashabiki wako wengi wanasema jamani Kalu tupatie hata nambari ya M-pesa tukutumie kitu. Wanakupenda hawa?" Jalango alisema

Kitendo hicho cha utu kiliweza roho ya mwanahabari huyo wa awali hadi akajipata akitokwa na machozi mahojiano yalipokuwa yanaendelea.

Kwa sasa Kalu ameweza kujikimu tena na amefungua studio ya kurekodi muziki ambapo anasaidia wengine kurekodi.

Alipokuwa anazungumza na Mpasho, Lolani aliwashukuru wote ambao walimsaidia kwa wakati huo.

"Kwa sasa niko na studio na camera za kurekodi na kuweza kuripoti nazo" Kalu alisema.

Alisema kuwa amerekodi nyimbo zake kadhaa ingawa hajarekodi video za nyimbo hizo bado.

"Nimeandika kitabu cha muziki kwa Kiswahili ambacho kinaitwa 'Mawe Saba'. Ningeomba wizara ya elimu iweze kukitumia shuleni kwenye mafunzo ya muziki. 

Pia nimerekodi nyimbo na ningewaomba wanisaidie kurekodi video. Niko na wimbo ambao unazungumzia umuhimu wa kushirikiana kama taifa.

Nawaomba muweze kujiunga na akaunti yangu wa Youtube, Lolani Media ili niweze kupata malipo kwenye mtandao huo" Lolani alisema.