SIMULIZI ZA HAMO NA JEMUTAI

Hamo asimulia alivyolazimika kulala ndani ya gari kwa miezi miwili kufuatia mzozo na Jemutai

Alisema kuwa kuingia kwa janga la Corona pia kulichangia maamuzi yake ya kulala ndani ya gari

Muhtasari

•Hamo alisema kuwa angetoka kazini mwake Royal Media na kujipatia malazi ndani ya gari lake hadi mapema mwaka uliopita.

•Alisema kuwa kazi zake za kando ambazo zilikuwa zinamletea mapato makubwa zilikuwa zimekwama. 

Jemutai & Hamo
Jemutai & Hamo
Image: Instagram// Jemutai

Mcheshi Herman Kago almaarufu kama Profesa Hamo amefichua kuwa alilala ndani ya gari yake kwa miezi miwili baada ya kukosana na mpenzi wake Jemutai.

Hamo alisema kuwa angetoka kazini mwake Royal Media na kujipatia malazi ndani ya gari lake hadi mapema mwaka uliopita.

Licha ya kuwa na kazi yenye mapato mazuri, Hamo aliamua kulala ndani ya gari baada ya kumuachia Jemutai nyumba ambayo walikuwa wakiishi pamoja na watoto wao wawili.

Alisema kuwa kuingia kwa janga la Corona pia kulichangia maamuzi yake ya kulala ndani ya gari.

"COVID 19 ilikuwa imetokea, mshahara ikakatwa na bado nilikuwa na madeni. Benki ni zile zile, lazima ulipe. Kazi zetu za kando kando hazikuwepo, hungeenda mahali. Pesa nilizokuwa napata aidha  nilipe madeni, niwekeze kwa biashara na nipate pesa kidogo ya kununua mafuta nisonge" Hamo alisema.

Alifichua kuwa aliukuwa anaenda kwa ukumbi wa mazoezi ili aweze kupata kuoga kisha alale kwa gari lake.

"Wadhani nilienda kwenye ukumbi wa mazoezi kwa sababu nilipenda kujiweka sawa? Hapana, hiyo ndiyo ilikuwa bafu yangu" Hamo alisema.

Alisema kuwa kazi zake za kando ambazo zilikuwa zinamletea mapato makubwa zilikuwa zimekwama.

Wapenzi hao wawili walikuwa  wakisimulia kuhusu safari yao ya mapenzi kwenye kipindi cha 'Raw & Candid' katika mtandao wa YouTube.

Kulingana na wawili hao, mzozo ulikuwa umeibuka baada ya Jemutai kuhudhuria sherehe bila idhini yake Hamo.

Jemutai alikuwa amemuarifu Hamo kuwa alikuwa amealikwa na rafiki yake kuhudhuria sherehe ya kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa. Hamo hakukubaliana naye na hakupendezwa na mpango huo.

Baada ya mazungumzo, Jemutai akamwambia Hamo kuwa ameamua hatahudhuria sherehe hiyo na wakamalizana. Hata hivyo, Jemutai alikaidi msimamo wake na akaenda. Jambo hilo halikumfurahisha Hamo.

"Wewe mwenyewe uliniambia kuwa hutaenda, maneno yako. Kesho yake nilipoenda kupiga picha na Doc nikapigiwa na mwenye sherehe akaniambia kuwa bibi yangu ako pale. Nikashindwa vipi na hukuwa umeniambia" Hamo alimwambia Jemutai.

Jemutai alisema kuwa alibadilisha mawazo na kuenda kusaidia rafiki yake kupanga sherehe alipata ikiwa imeshika na akaamua kukaa. Hamo naye kwa hasira akaamua kupiga sherehe pia.

Asubuhi iliyofuata walipopatana kwa nyumba Jemutai aliamua kuwa ataenda ila Hamo akaamua kuenda mwenyewe na kuwaachia nyumba.

Baada ya kuondoka pale Hamo aliishi ndani ya gari lake kwa miezi miwili.