Daktari alipendekeza mwanamuziki King Kaka afanyiwe vipimo vya saratani- Nana Owiti afichua

Muhtasari

•Bi Owiti amefichua kwamba daktari aliyekuwa anahudumia King Kaka alipendekeza vipimo vya saratani kwani dalili ambazo mwanamuziki huyo alikuwa anaonyesha zilienda kukaribia za ugonjwa huo ambao unaogopwa sana duniani kutokana na madhara yake.

•Owiti alikesha usiku kucha akiwaza ilhali King Kaka mwenyewe alilala usingizi wa pono kama mtu aliye buheri wa afya licha ya kuwa mwili wake ulikuwa umedhoofika.

Image: INSTAGRAM// KING KAKA

Mwanamuziki mashuhuri wa nyimbo za kufoka Kennedy Ombima amekuwa akiugua kwa kipindi cha miezi minne ambayo imepita.

Haijathibitishwa wazi maradhi ambayo msanii huyo amekuwa akiugua kwani angali ameweka habari hizo kama siri.

Hata hivyo mke wa rapa huyo, Nana Owiti amefunguka kuhusu masaibu ambayo alipitia wakati hali ya afya ya mumewe ilikuwa imedhoofika.

Bi Owiti amefichua kwamba daktari aliyekuwa anahudumia King Kaka alipendekeza vipimo vya saratani kwani dalili ambazo mwanamuziki huyo alikuwa anaonyesha zilikaribia kufanana na za ugonjwa huo ambao unaogopwa sana duniani kutokana na madhara yake.

"Nakumbuka wakati daktari alipendekeza tufanye vipimo vya saratani. Kwa kweli alikuwa na sababu zake, namaanisha ulionyesha dalili zote na jambo hilo liliibua mawazo mengi  ya shida kichwani mwangu" Bi Owiti alisema.

Ingawa jambo hilo lilimnyima  usingizi bi Owiti, mumewe kwa upande wake hakuonyesha dalili zozote za mtu mwenye hofu

Owiti alikesha usiku kucha akiwaza ilhali King Kaka mwenyewe alilala usingizi wa pono kama mtu aliye buheri wa afya licha ya kuwa mwili wake ulikuwa umedhoofika.

"Sielewi ulivyoweza kulala kabisa usiku huo. Yaani unaenda kupimwa saratani mwilini asubuhi ifuatayo na unalala usiku kucha. Nataka kufunzwa" Bi Owiti alisema.

Wawili hao waliandamana hadi hospitali siku iliyofuata na vipimo hivyo vikafanyiwa. Hata hivyo hawaweka wazi matokeo ya vipimo vilivyofanyiwa.

Kwa upande wake King Kaka alimshukuru mkewe kwa kusimama naye katika wakati huo mgumu na kumweleza kuwa neema za Maulana ndizo zilimuwezesha kutokuwa na wasiwasi baada ya daktari kupendekeza vipimo vya saratani.

"Elekeza wasiwasi wako kwake kwa sababu anatujali, lakini usingizi ikikuja unalala tu.Siwezi kushukuru vya kutosha. Tutaendelea kuomba" King Kaka alimjibu mkewe.

Mapema wiki hii Bi. Owiti alihakikishia mashabiki kwamba King Kaka anaendelea kupata afueni na tayari ameongeza kilo 6 baada ya kupoteza kilo 33 katika kipindi alichokuwa amelemewa na maumivu.