'Mmekuwa mkinionyesha mapenzi makubwa sana,' Harmonize kutumbuiza katika miji 10 Kenya Desemba kama ishara ya shukrani

Muhtasari

•Harmonize ambaye amekuwa kwenye ulingo wa sanaa kwa zaidi ya mwongo mmoja uliopita  amewashukuru sana  mashabiki wake wote kutoka Kenya huku akitangaza kuwa atakuwa akifanya ziara nchini hivi karibuni.

•Harmonize amekiri kwamba Wakenya wamekuwa guzo muhimu sana katika taaluma yake ya kutengeneza na kucheza muziki.

Image: INSTAGRAM// HARMONIZE

Nyota wa muziki kutoka Tanzania Rajab Abdul Kahali almaarufu kama Harmonize ameridhishwa sana na upendo mkubwa ambao  amekuwa akionyeshwa na Wakenya.

Harmonize ambaye amekuwa kwenye ulingo wa sanaa kwa zaidi ya mwongo mmoja uliopita  amewashukuru sana  mashabiki wake wote kutoka Kenya huku akitangaza kuwa atakuwa akifanya ziara nchini hivi karibuni.

Kupitia kurasa zake za mitandao ya Kijamii, Harmonize ametangaza kwamba atafanya tamasha katika angalau miji kumi nchini mwezi Desemba kama ishara ya shukrani kwa mashabiki wake kutoka Kenya.

Harmonize amekiri kwamba Wakenya wamekuwa guzo muhimu sana katika taaluma yake ya kutengeneza na kucheza muziki.

"Desemba nchini Kenya. Siwezi kusubiri. Mmekuwa mkinionyesha mapenzi kwa kiasi kikubwa sana tangu nilipoanza safari ya muziki. Nimechagua hii Desemba kuja kuwalipa fadhira najitahidi kila niwezavyo angalau miji mikubwa 10. Nifike uwanja mmoja hadi mwingine" Diamond amesema.
Hali kadhalika staa huyo wa Bongo ameahidi kushirikisha wasanii kadhaa katika EP yake mpya anayotazamia kupatia jina 'Gengefleva'

"Sitoangalia ukubwa wala udogo wa msanii. Lengo ni kuunganisha muziki wa Tanzania na Kenya. Tafadhali mnitajie msanii unayemkubali ambaye unajua tukikutana kwenye ngoma kinawaka" Harmonize amesema.

Harmonize amesema kwamba tiketi za  tamasha yake zitakuwa tayari wiki ijayo huku akitangaza kuwa tamasha ya kwanza itafanyika mjini Kakamega.