Muigizaji Jackie Matubia afichua sababu za kulazwa hospitalini

Muhtasari

•Matubia amefichua kwamba alilazimika kulazwa hospitalini baada ya kukumbwa na uchungu kwenye tumbo lake.

•Baada ya kufanyiwa vipimo ilibainika kwamba mwigizaji huyo alikuwa amepatwa na uchungu wa uzazi usio halisi.

Image: INSTAGRAM// JACKIE MATUBIA

Mwigizaji mashuhuri Jackie Matubia anaendelea kupokea matibabu hospitalini baada ya kulazwa.

Matubia amefichua kwamba alilazimika kulazwa hospitalini baada ya kukumbwa na uchungu kwenye tumbo lake.

Kupitia kanda ya video ambayo alipakia Instagram, Matubia ambaye kwa sasa ni mjamzito ameeleza kwamba siku chache zilizopita daktari wake alimshauri akimbie hospitalini baada ya kumweleza dalili alizokuwa nazo.

"Tulipokewa kwa dharura. Madaktari waliangalia mapigo ya moyo ya mtoto. Mtoto alikuwa sawa. Nashukuru Mungu," Alisema.

Baada ya kufanyiwa vipimo ilibainika kwamba mwigizaji huyo alikuwa amepatwa na uchungu wa uzazi usio halisi.

"Waliangalia kama seviksi yangu ilikuwa imefunguka. Nashukuru Mungu kwamba haikuwa imefunguka. Walianza kunitibu ili kuhakikisha uchungu huo umeenda, seviksi haijafunguka na mimi pamoja mtoto wangu tuko sawa," Alisema.

Mwigizaji huyo wa Zora aliweka wazi kwamba bado hajajifungua. Aliwahakikishia mashabiki wake kwamba atakuwa anapewa ruhusa kutoka hospitalini hivi karibuni.

Hapo awali alikuwa amepakia video iliyoonyesha akiwa hospitalini na mume wake Blessing Lung'aho.