Wema Sepetu afunguka hamu yake kuvunja utasa na kupata mtoto wa kiume

"Ata mimi natamani mtoto wa kiume. Sijui mbona watu hawaelewi hivyo," Wema alisema.

Muhtasari

•Mpenzi huyo wa zamani wa Diamond Platnumz aliweka wazi kuwa pia yeye anatamani sana kupata mtoto wa kiume.

•Hapo awali aliwahi kufunguka kuhusu  tatizo kwenye tumbo lake la uzazi linalomzuia kushika ujauzito.

Image: INSTAGRAM// WEMA SEPETU

Hivi majuzi, muigizaji Wema Sepetu alimkaribisha mwimbaji Tuerny katika kipindi chake cha Cook With Wema kwenye mtandao wa YouTube.

Katika kipindi hicho cha mazungumzo ya wazi, mastaa hao wawili wa Bongo ambao kwa kiasi fulani wanakaribia kufanana walizungumza kuhusu masuala mbalimbali kuanzia umaarufu, mahusiano, kazi, malengo n.k.

Tuerny alifichua kwamba moja ya malengo yake makubwa mwaka huu ni kupata mtoto wa kiume na mpenzi wake.

"Naolewa. Mwaka huu Mungu akinijalia naweza nikapata mtoto. Natamani mtoto wa kiume,"  alisema mwimbaji huyo.

Ni wakati huo ambapo Wema Sepetu aliweka wazi kuwa pia yeye anatamani sana kupata mtoto wa kiume.

"Ata mimi natamani mtoto wa kiume. Sijui mbona watu hawaelewi hivyo," alisema.

Hii sio mara ya kwanza kwa mpenzi huyo wa mwimbaji Whozu kufunguka kuhusu hamu yake ya kupata mtoto. Mara kadhaa, Wema ambaye hajafanikiwa kupata mtoto hata mmoja kufikia sasa ameeleza nia yake ya kuwa mama.

Mwezi Desemba, mpenzi huyo wa zamani wa bosi wa WCB, Diamond Platnumz alimuomba Maulana amjalie mtoto siku moja.

Wema aliandika ujumbe huo chini ya picha yake akiwa amemshika mtoto mchanga ambayo alipakia kwenye Instagram.

"Eh Mungu tafadhali nibariki na wangu siku moja🙏🙏🙏," alisema.

 Alikiri kwamba kumtazama mtoto huyo mchanga mikononi mwake kulimfanya ajisikie kuwa kuenda naye awe wake.

"Nilitamani nikimbie naye wallahy🥺🥺🥺" alisema.

Hadi wa leo, Wema Sepetu ambaye ana umri wa miaka 32 bado hajaweza kumshika mtoto kutoka tumboni mwake.

Kwa miaka mingi, muigazaji huyo amekuwa akishambuliwa na kukejeliwa mitandaoni kutokana na hali yake. Wengine hata hivyo wamekuwa wakimfariji na kumtia moyo mpenzi huyo wa zamani wa Diamond.

Takriban miaka minne iliyopita Wema aliwahi kufunguka kuhusu  tatizo kwenye tumbo lake la uzazi linalomzuia kushika ujauzito.

“Unajua mimi nilikuwa na tatizo kubwa sana kwa upande wa tumbo langu la uzazi lililosababisha nisiweze kuzaa kwa muda wote huu. Ngoja niweke wazi leo watu wajue, mimi nina ugonjwa ambao unasababisha mayai yangu ya uzazi kutoboka na kushindwa kupevusha mbegu za uzazi," Alisema katika mahojiano na Global Publishers.

Licha ya kuwa na tatizo kwenye tumbo la uzazi, muigizaji huyo mwenye sauti nzuri kweli amekuwa akionyesha wazi kuwa bado hajapoteza matumaini ya kuwahi kukumbatia mtoto wake kuzaa katika siku za usoni.