"Kila mtu akae kwake!" Akothee afichua sababu ya baadhi ya wanafamilia kutohudhuria harusi yake

Akothee amedokeza kuwa alikosa kuwaalika baadhi ya wanafamilia wake kimakusudi.

Muhtasari

•Akothee aliweka wazi kuwa baadhi ya watu ambao wengi wangedhani wangekuwepo kwenye hafla hiyo hawakuonekana kwa sababu hakuwaalika.

•Alishauri watu dhidi ya kutumia hafla muhimu kama jukwaa la upatanisho baina ya wanafamilia wanaozozana.

Akothee na mume wake Denis Shweizer
Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwimbaji na mjasiriamali Esther Akoth almaarufu Akothee amedokeza kuwa alikosa kuwaalika baadhi ya wanafamilia wake kimakusudi.

Akizungumza kwenye ukurasa wake wa Instagram siku ya Jumapili, mama huyo wa watoto aliweka wazi kuwa baadhi ya watu ambao wengi wangedhani wangekuwepo kwenye hafla hiyo hawakuonekana kwa sababu hakuwaalika.

"Nilifurahia harusi yangu. Hasa wakati wa kuchagua orodha ya wageni. (Kama hukuwaona jua hawakualikwa). Ilikuwa sehemu bora zaidi yake. Nilikuwa na watu tu ambao nilitaka kuwa nao," Akothee aliandika siku ya Jumapili.

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 aliwashauri watu kuwaweka wanafamilia mahali wanapostahili kila mara.

Alishauri watu dhidi ya kutumia hafla muhimu kama jukwaa la upatanisho baina ya wanafamilia wanaozozana.

"Kama mbaya mbaya, kila mtu akae kwake. Tena, msamaha sio lazima uwe hadharani, hiyo ni kujifanya. Kwanza jisamehe kisha uwasamehe wengine," alisema.

Aliongeza, "Kuweka familia kama familia haimaanishi ni lazima muwe marafiki au muwe karibu, usilazimishe mambo na familia, wao ni familia, iweke familia. Kuna mahali kwingi ambako mtakutana k.m kwenye mazishi." 

Mjasiriamali huyo alibainisha kuwa mtu anapolazimisha urafiki katika familia huishia kuumizwa ama kuvunjana moyo.

"Kumbuka hamjuani ndio maana unaona Kaini alimuua Habili, Yusufu aliuzwa na ndugu zake mwenyewe, sasa wewe ni nani?"

Akothee na mchumba wake Dennis Shweizer almaarufu Mister Omosh walifunga pingu za maisha katika harusi ya kifahari iliyofanyika Windsor Golf Hotel & Country Club, jijini Nairobi mnamo Aprili 10.

Harusi ya mama huyo wa watoto watano ilipambwa na wanafamilia, marafiki wa karibu, wasanii maarufu na wanasiasa mashuhuri nchini. Jumla ya watu wasiopungua mia tatu walikuwa wamealikwa kwenye hafla hiyo.

Dada mdogo wa Akothee, Cebbie Koks, ambaye anafahamika kuwa na ugomvi naye hata hivyo hakuonekana kwenye hafla hiyo.

Akihutubia wanahabari baada ya kutua kutoka Ufaransa, mwimbaji huyo aliweka wazi kuwa ni wanawe wawili pekee, Prince Ojwang na Prince Oyoo ambao hawangefanikiwa kufika kwenye harusi hiyo kutokana na shule lakini akadokeza watashuhudia sherehe ya pili itakayofanyika Uswizi mnamo Julai 10.

"Karibu Prudence Vanpelt, bintiye Akothee. Msilete propaganda na siasa za familia kwa harusi yangu. Watu pekee ambao watakosa harusi yangu ni wanangu wawili ambao hawatafanikiwa kwa sababu ya sheria za shule, lakini watashuhudia ambayo imeratibiwa kufanyika Julai 10. Mwaka mzima Akothee anaolewa," alisema.

Mwezi Oktoba, msanii huyo mwenye umri wa miaka 43 alifunguka kuhusu ugomvi wake na Cebbie na kutangaza hatakuwa akihudhuria hafla zake na vilevile watu wasitarajie kumuona  dadake huyo katika hafla yake.