Akothee afunguka kuhusu kufunga ndoa na wanaume kadhaa hapo awali

Akothee aliweka wazi kuwa ndoa yake na Omosh ni ya pili kwa kuwa mahusiano mengi ya awali hayakufikia ndoa rasmi.

Muhtasari

•Akothee aliwataka mashabiki wake kutoamini tetesi nyingi zisizo na msingi wanazoona kwenye mtandao ya kijamii.

•Aliongeza, "Wanaume hawa wawili wanaishi Afrika Kusini. Mzungu ameoa na ana familia. Kuweni na adabu."

Image: HISANI// AKOTHEE

Mwanamuziki Esther Akoth almaarufu Akothee, kwa mara nyingine amesisitiza kuwa amewahi kuolewa rasmi mara mbili pekee.

Katika taarifa yake siku ya Alhamisi, mama huyo wa watoto watano aliweka wazi kwamba ndoa yake na Denis Shweizer almaarufu Bw Omosh  ni ya pili kwa kuwa mahusiano yake mengi ya awali hayakufikia ndoa rasmi.

Akothee aliwataka mashabiki wake kutoamini tetesi nyingi zisizo na msingi wanazoona kwenye mtandao ya kijamii.

"Kwa wafuasi wangu wapya, msiingie kwenye mtego wa watu wenye wivu. Nimeolewa mara moja tu na mahusiano ambayo hayakuweza kufika kwenye ndoa 🤣🤣🤣🤣,hii ni ndoa yangu ya pili," alisema kwenye Instagram.

Mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 43 alitaja madai mengi kuhusu yeye kuolewa mara kadhaa kuwa uwongo.

Alikana kuwahi kufunga pingu za maisha na wanaume wawili wa Afrika Kusini ambao amewahi kuhusishwa nao katika siku za nyumba huku akibainisha kuwa walikuwa wahusika tu katika video za nyimbo zake.

"Hawa ni vixens kwenye video zangu za muziki. Jisajili kwa chaneli yangu ya YouTube na utazame nyimbo zangu kabla ya kujiaibisha, Oyuech Sweetlove ft diamond na Yuko moyoni ambazo zilirekodiwa  Afrika Kusini," alisema.

Aliongeza, "Wanaume hawa wawili wanaishi Afrika Kusini. Mzungu ameoa na ana familia. Kuweni na adabu.

Akothee alitaka watu wenye nia mbaya dhidi yake waachane naye.

Akothee na mchumba wake Dennis Shweizer almaarufu Mister Omosh walifunga pingu za maisha katika harusi ya kifahari iliyofanyika Windsor Golf Hotel & Country Club, jijini Nairobi mnamo Aprili 10.

Harusi ya mama huyo wa watoto watano ilipambwa na wanafamilia, marafiki wa karibu, wasanii maarufu na wanasiasa mashuhuri nchini. Jumla ya watu wasiopungua mia tatu walikuwa wamealikwa kwenye hafla hiyo ya kukata na shoka. Ilikuwa ni harusi ya Akothee  ya pili kwani alifunga ndoa kwa mara ya kwanza na baba ya binti zake watatu, Bw Jared Okello zaidi ya mwongo mmoja uliopita. 

Hapo awali, msanii huyo mwenye umri wa miaka 43 aliwahi kufichua harusi yake na Bw Jared iligharimu shilingi  2,500 pekee.