Wakati Fred Omondi alikosoa kanisa "Ukifiwa, marafiki kutoka baa watakupa milioni. Wa kanisa watakupa maombi"

"Watu wengi wazuri hawako kanisani. Kanisa ni mahali pazuri, sina suala nalo, lakini watu wengi wazuri hawapo," Fred alisema.

Muhtasari

•Marehemu alikiri kuhusu kuokoka na kuzungumzia jinsi anavyotazama wokovu kwa njia tofauti na watu wengine.

•Alisema kwamba kuna mambo mbadala bora ambayo watu wanaweza kufanya kuliko kwenda kuimba kanisani wiki nzima.

Image: INSTAGRAM// FRED OMONDI

Marehemu Fred Omondi, kaka ya mchekeshaji na mwanaharakati Eric Omondi, alijitokeza kwenye mahojiano takriban miaka mitatu iliyopita na kuzungumzia suala la wokovu.

Akizungumza na mtangazaji Oga Obinna kwenye KulaCoolerShow, marehemu alikiri kuhusu kuokoka na kuzungumzia jinsi anavyotazama wokovu kwa njia tofauti na watu wengine.

Alionekana kulalamika kuhusu baadhi ya masuala katika kanisa akibainisha kuwa kuna unafiki kwenye jukwaa hilo ambalo mara nyingi hutambuliwa kama nyumba ya Mungu.

“Kusema nimeokoka, ina maana tofauti. Ninaamini katika Mungu, daima nimemwamini Mungu. Lakini kwa kile ninachokiona hata kutoka kwa watu waliookoka, ningependelea kuwa na watu wa baa,” Fred alisema.

Aliongeza, “Ukipata msiba, marafiki zako wa baa watakupa milioni. Kutoka kanisani watakupa maombi na kwaya. Kisha utalazimika kumlipa mchungaji kwa kuja kwenye mazishi. Watu wengi wazuri hawako kanisani. Kanisa ni mahali pazuri, sina suala nalo, lakini watu wengi wazuri hawapo. Wanaojifanya wote wako kwa kanisa.”

Alisema kwamba kuna mambo mbadala bora ambayo watu wanaweza kufanya kuliko kwenda kuimba kanisani wiki nzima kuanzia Jumatatu hadi Jumapili.

“Wakati huo enda tu kwa nyumba za Watoto. Bariki mtu. Enda ata ujue Jirani yako. Wengine hawajui majirani zao. Hicho ni kitendo cha wema,” alisema.

Fred aliaga dunia siku ya Jumamosi asubuhi katika kile kilichoripotiwa kuwa ajali mbaya ya barabarani iliyotokea kwenye barabara ya Outering jijini Nairobi.

Polisi walisema ajali iliyomuua Fred ilitokea Jumamosi asubuhi baada ya bodaboda iliyokuwa imembeba kugongwa na basi lililokuwa likienda mwendo kasi na kumlazimisha mwendeshaji huyo na marehemu kutua kwenye lami.

Omondi alikimbizwa katika Hospitali ya Mama Lucy ambapo alitangazwa kuwa amefariki alipokuwa akihudumiwa, afisa wa polisi alisema.

Shahidi alisema alifariki papo hapo.

Marafiki na watu mashuhuri waliotumbuiza naye walikusanyika kwenye mitandao ya kijamii kuomboleza kifo chake.

Mchekeshaji Terrence Creative alipokuwa akimuomboleza alisema alipokea simu saa kumi na mbili asubuhi Jumamosi kumjulisha kifo chake.

"Fred namshukuru Mungu kwa muda aliotupa pamoja bro, umekuwa sehemu ya kazi yangu na ukuaji katika tasnia. Ulinichukulia kama kaka na kunikaribisha wakati sikuwa na mahali pa kwenda," Terrence alisema.

"Ulinipa jukwaa na kunilipa, na kwa pamoja tulianza maonyesho ya vichekesho vya klabu. Nitathamini kila wakati tuliposhiriki jukwaa."

Mwanasiasa Millicent Omanga, alitoa rambirambi zake kwa X, akisema:

"Tasnia ya ubunifu imepoteza thamani. Fred Omondi aliangaza vyumba vyetu vya kuishi na vichekesho vyake vya uraibu. Kwamba amepoteza maisha yake katika ajali ya barabarani inahuzunisha moyo. Ninawapa pole familia yake, marafiki, na mashabiki wake. Naomb nafsi yake ipate amani kamili."

Mwanamuziki Nameless naye alimlilia.

“Hii imezidi... maisha ni tete! Pumzika vizuri Fred! Habari za kusikitisha kama hizo! Pole za dhati kwa familia!!